Marekani yaendeleza siasa za kibeberu Syria
Mtaalamu mmoja wa masuala ya kisiasa wa nchini Marekani amesema kuwa, nchi hiyo inaendeleza siasa za kibeberu nchini Syria licha ya Donald Trump kuonesha wakati wa kampeni za uchaguzi kuwa hatojiingiza sana katika masuala ya ndani ya Syria.
Myles Hoenig amesema hayo leo katika mahojiano na Press TV na kuongeza kuwa, shabaha ya Washington nchini Syria ni kuwabebesha wananchi wa nchi hiyo ya Kiarabu siasa zake za kibeberu, ingawa hata hivyo siasa hizo hadi hivi sasa zimefeli.
Mtaalamu huyo wa masuala ya kisiasa wa Marekani amesema, Washington na waitifaki wake katika vita dhidi ya wananchi wa Syria wamefanya mauaji makubwa ya kuangamiza kizazi, ukatili ambao wameufanya pia nchini Iraq.
Amesema, mauaji ya umati yanayofanywa na Marekani duniani bila ya shaka yoyote ni jinai ya kivita na ni uhalifu dhidi ya binadamu.
Ikumbukwe kuwa, tarehe 7 Aprili mwaka huu, Marekani ilishambuliwa kwa makombora ya Tomahawk, kituo cha jeshi la anga cha Syria cha Shayrat katika mkoa wa Homs, baada ya kuona magenge ya kigaidi yanayoungwa mkono na Marekani na vibaraka wake yanazidi kuelemewa na kupata pigo nchini humo. Marekani ilifanya mashambulizi hayo ya kivamizi baada ya kudai kuwa eti jeshi la Syria limetumia silaha za kemikali dhidi ya magenge yakigaidi.
Shambulio hilo la Marekani lilifanyika kabla ya hata kufanyika uchunguzi wowote kuhusiana na madai hayo ya Marekani, huku wataalamu wa Umoja wa Mataifa wakithibitisha kuwa serikali ya Syria haina tena silaha za kemikali.