Wazayuni wamzuia Waziri wa Mambo ya Nje wa Indonesia kuingia Palestina
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i2995-wazayuni_wamzuia_waziri_wa_mambo_ya_nje_wa_indonesia_kuingia_palestina
Utawala wa kizayuni wa Israel umemzuia Waziri wa Mambo ya Nje wa Indonesia, Retno Marsudi kuingia katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu, ambapo alitazamiwa kukutana na kufanya mazungumzo na viongozi wa Palestina.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Mar 14, 2016 01:24 UTC
  • Wazayuni wamzuia Waziri wa Mambo ya Nje wa Indonesia kuingia Palestina

Utawala wa kizayuni wa Israel umemzuia Waziri wa Mambo ya Nje wa Indonesia, Retno Marsudi kuingia katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu, ambapo alitazamiwa kukutana na kufanya mazungumzo na viongozi wa Palestina.

Taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Palestina imesema kuwa, wazayuni maghasibu wamekataa kumruhusu Marsudi kuingia mjini Ramallah, huko Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan ambapo alitazamiwa kukutana na Mahmud Abbas, Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina na mwenzake Riyadh al-Maliki. Kadhalika Waziri wa Mambo ya Nje wa Indonesia alitazamiwa kufungua ofisi ya ubalozi mdogo wa Indonesia mjini Ramallah. Taarifa hiyo ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Palestina imeongeza kuwa, badala yake, Waziri wa Mambo ya Nje wa Indonesia atakutana na mwenzake wa Palestina katika nchi jirani ya Jordan.

Vyombo vya habari vya utawala haramu wa Israel vimeripoti kuwa, Marsudi amezuiwa kukutana na viongozi wa Palestina baada ya kukataa kukutana na maafisa wa utawala huo ghasibu.

Haya yanajiri siku chache baada ya Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) kutoa wito wa kususiwa bidhaa zinazozalishwa na utawala haramu wa Israel katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu. Taarifa hiyo ilitolewa mwishoni mwa kikao cha tano cha dharura cha wakuu wa (OIC) kilichofanyika hivi karibuni katika mji mkuu wa Indonesia, Jakarta.