Kufichuliwa ushiriki wa Imarati katika vitendo vya kigaidi vya Israel
Habari mbalimbali zimearifu tukio jipya la namna Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati) unavyoshiriki katika vitendo vya kigaidi vya utawala wa Israel; suala ambalo katika siku za hivi karibuni kwa mara nyingine tena limeakisi ushirikiano uliopo kati ya watawala wa Kiarabu na maghasibu wanaoikalia Quds Tukufu kwa mabavu katika kuwakandamiza wananchi wa Palestina na kusogeza mbele siasa za kigaidi za Israel.
Taasisi ya Kiarabu ya Kutetea Haki za Binadamu ya nchini Uingereza imefichua kuwa watu wasiopungua wawili wanachama wa timu iliyohusika na mauaji ya Mahmoud al Mabhouh mmoja wa viongozi wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) wanaishi Imarati wakiwa huru na bado hawajafikishwa mbele ya vyombo vya sheria. Taasisi hiyo ya Kiarabu ya Haki za Binadamu imesisitiza katika taarifa yake kwamba, waliomuua Mahmoud al Mabhouh walikimbilia Jordan baada ya kutekeleza mauaji hayo, amma maafisa wa Jordan waliwakabidhi wauaji hao kwa maafisa wa Imarati. Mahmoud al Mabhouh aliuliwa tarehe 19 Januari mwaka 2010 akiwa katika hoteli moja huko Dubai akiwa na umri wa miaka 50. Imeelezwa kuwa maajenti wa Shirika la Ujasusi la Israel (MOSAD) walitekeleza oparesheni hiyo ya mauaji kwa kuingia katika hoteli alimokuwa akiishi Mabhuh huko Dubai na kisha kumuua kwa kumdunga sindano ya sumu.
Uhusiano wa siri na wazi kati ya utawala wa Kizayuni na baadhi ya nchi za Kiarabu khususan nchi za Kiarabu za Ghuba ya Uajemi ni miongoni mwa uhakika wa mambo ambao siku zote umekuwa ukiakisiwa na vyombo mbalimbali vya habari. Kuhusiana na suala hilo, Kanali ya Habari ya al Jazeera yenye makao yake nchini Qatar pia ilijaribu kufichua namna Imarati ilivyohusika katika kuumua Mahmoud al Mabhouh huko Dubai. Kwa mujibu wa nyaraka na vithibitisho vilivyopo, watu wawili kutoka timu iliyohusika na mauaji ya Mabhuh waliachwa huru na maafisa wa Imarati kutoka jela za nchi hiyo miaka saba kabla ya kutekelezwa mauaji hayo huko Dubai. Watuhumiwa waliotajwa mara kwa mara walikuwa wakikutana na mmoja wa maajenti wa Mosad kwa mujibu wa picha zilizorekodiwa huko Dubai.
Maajenti wa ujasusi na ugaidi wa Israel hadi kufikia sasa wametekeleza mauaji mengi nje na ndani ya maeneo ya Palestina yanayokaliwa kwa mabavu; ambapo mifano ya mauaji hayo ni pamoja na kuuliwa Fat'h Shaqiq Mwasisi wa Harakati ya Jihadul Islami ya Palestina katika kisiwa cha Malta mwezi Oktoba mwaka 1995, kuuawa huko Syria Imad Mughuniya mwanachama wa ngazi ya juu wa chama cha Hizbullah cha Lebanon mnamno mwaka 2008 na kuuawa Sheikh Ahmad Yassin Mwasisi wa Harakati ya Hamas huko Ukanda wa Ghaza.
Khalid Mash'al mmoja wa maafisa wa Hamas pia alinusurika kuuliwa akiwa Jordan mwaka 1997. Uchunguzi uliofanywa kuhusu oparesheni za kigaidi zinazofanywa na Israel umeonyesha kuwa moja ya vituo vya kupanga na kuendeshea oparesheni hizo kilikuwa nchini Imarati. Imeelezwa kuwa miji mbalimbali ya pambizoni mwa eneo la Ghuba ya Uajemi ilikuwa sehemu za kuwahifadhia majasusi na magaidi wa utawala wa Kizayuni kufuatia kuimarika uhusiano kati ya Umoja wa Falme za Kiarabu na utawala wa Kizayuni katika miongo miwili iliyopita. Hakuna kizuizi chochote kinachowazuia maajenti wa Israel kutekeleza siasa za ugaidi katika eneo la Mashariki ya Kati kutokana na uungaji mkono na msaada wanaopewa na wakuu wa Imarati na ule wa vyombo vya usalama na sheria vya Jordan.
Oparesheni nyingi za kigaidi za utawala wa Kizayuni zimeratibiwa na kufuatiliwa huko Dubai na Abu-dhabi; na ni wazi kwamba Imarati imegeuka na kuwa kituo cha oparesheni hizo za kijasusi na kigaidi za Israel katika eneo. Weledi wa mambo wanamini kuwa utawala wa Kizayuni ambao umejengeka katika misingi ya ugaidi, vitendo vya mabavu na kupenda kujitanua haujawahi kufikishwa mbele ye vyombo vya kimataifa kutokana na uungaji mkono wa pande zote wa nchi za Magharibi na khususan Marekani na vile vile misimamo inayoonyeshwa na watawala wa nchi za Kiarabu katika kufunika vitendo vya kigaidi vinavyotekelezwa na utawaa huo haramu. Hatua na misimamo kama hiyo ndiyo inayozidi kuupa kiburi utawala wa Kizayuni kuendeleza jinai zaidi katika eneo kila uchao. Israel inashadidisha siasa zake hizo za ugaidi lengo likiwa ni kuzusha hofu na wahka na kuzima harakati yoyote ya muqawama katika Mashariki ya Kati inayokabiliana na utawala huo ghasibu. Aidha watawala wa Kiarabu ambao hawana uungaji mkono wowote wa wananchi katika eneo wanayatazama makundi ya mapambano dhidi ya Uzayuni katika eneo hili kama tishio kwao. Siasa hizo mbovu za viongozi wa Imarati na kufichuliwa ushirikiano wao na Israel kumeyumbisha zaidi nafasi ya watawala hao mbele ya fikra za waliowengi katika eneo hili.