Imarati na Saudia zakataa wito wa Qatar wa mazungumzo
Umoja wa Falme za Kiarabu umekataa wito uliotolewa hivi karibuni na Amir wa Qatar, Sheikh Tamin bin Hamad al-Thani, wa kufanyika mazungumzo ya kuupatia ufumbuzi mgogoro uliopo, na kusisitiza kuwa Doha sharti ibadili sera zake kabla ya kufanyika jitihada zozote za kuiondolea vikwazo nchi hiyo ndogo ya Ghuba ya Uajemi, iivyowekewa na Saudia na wapambe wake.
Anwar Gargash, Waziri wa Mambo ya Nje wa Imarati amesema iwapo Qatar inataka kufanyike mazungumzo ya kuiondolea vikwazo, lazima ichukue hatua za mabadiliko.
Hata hivyo hajatoa maelezo zaidi kuhusu mabadiliko hayo anayotaka yafanywe na Qatar.
Mwezi uliopita, Qatar iliapa kutotekeleza orodha ya masharti 13 ya nchi za Kiarabu, kukiwemo kufunga kanali ya televisheni ya al-Jazeera, kukata uhusiano na Iran na kufunga kituo cha kijeshi cha Uturuki kilichoko nchini humo.
Hii ni katika hali ambayo, Ijumaa iliyopita, Adel al-Jubeir, Waziri wa Mambo ya Nje wa Saudi Arabia alipokuwa katika ziara nchini Italia ailisisitiza kuwa, Doha haina budi kutii na kutekeleza masharti iliyoanishiwa na nchi nne za Kiarabu zikiongozwa na Saudia, iwapo inataka kuondolewa vikwazo ilivyowekewa vya ardhini, angani na baharini.
Saudia kwa kushirikiana na nchi tatu za Kiarabu, yaani Imarati, Bahrain na Misri zilikata uhusiano wa kidiplomasia na Qatar hapo tarehe tano mwezi uliopita wa Juni kwa madai kuwa serikali ya Doha inaunga mkono ugaidi, hatua ambayo ilienda sambamba na kuiwekea mzingiro wa kila upande nchi hiyo ya Kiarabu.