Jul 24, 2017 03:58 UTC
  • Erdogan: Waislamu hawawezi kufumbia macho mgogoro wa al-Aqsa

Rais Recep Tayyip Erdoğan wa Uturuki amekosoa vikali hatua kandamizi za usalama za utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Wapalestina katika mji wa Quds Tukufu na kusisitiza kuwa katu Waislamu hawawezi kunyamazia kimya jinai hizo.

Erdogan aliyasema hayo jana Jumapili mjini Istanbul kabla ya kuanza ziara ya kuzitembelea Saudi Arabia, Kuwait na Qatar.

Shirika la habari la Tasnim limemnukuu Erdogan akifafanua kuwa: "Hakuna mtu anataraji ulimwengu wa Kiislamu kufumbia macho na kutotoa majibu mbele ya kudhalilishwa wenzao wa Palestina, na kuzuiwa kuingia katika Haram Takatifu (Masjidul Aqsa)."

Hapo jana kupitia taarifa, Jumuiya ya Nchi za Kiarabu iliutahadharisha utawala wa Kizayuni wa Israel kwamba 'unacheza na moto' kutokana na kushadidisha ukandamizaji dhidi ya Wapalestina wa Quds Tukufu inayokaliwa kwa mabavu; huku Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ikisema kuendelea ukandamizaji huo kunaonyesha kuwa Palestina iliyodhulumiwa ingali kadhia ya kwanza ya Ulimwengu wa Kiislamu. 

Maandamano ya kuwaunga mkono Wapalestina yamefanyika sehemu mbalimbali ikiwemo London

Hii ni katika hali ambayo, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linatazamiwa kufanya kikao hii leo kujadili kadhia hiyo ya Quds, kutokana na ombi la Misri, Ufaransa na Sweden. 

Wapalestina watano wameuawa shahidi na makumi ya wengine kujeruhiwa baada ya Israel kushadidisha siasa zake za ukandamizaji dhidi ya Wapalestina katika Msikiti wa al-Aqsa, tangu tarehe 14 mwezi huu.

Tags