Karibu watu 40 wauawa katika hujuma ya kigaidi Kabul, Afghanistan
Habari kutoka Afghanistan zinaarifu kwamba, karibu watu 40 wameuawa na wengine 60 kujeruhiwa katika shambulio la kigaidi lililotokea leo mjini Kabul, mji mkuu wa nchi hiyo.
Mauaji hayo yametokea baada ya gaidi mmoja kujiripua ndani ya gari inayotajwa kuwa ilikuwa imetegwa mada za miripuko magharibi mwa mji wa Kabul. Polisi ya Afghanistan imesema kuwa, kuna uwezekano idadi ya wahanga wa hujuma hiyo ikaongezeka, kutokana na majeruhi wengi kuwa na hali mbaya.
Kwa kuzingatia kuwa eneo la magharibi mwa mji wa Kabul ni makazi ya Waislamu wa jamii ya Shia, inasadikiwa kuwa shambulio hilo limewalenga watu wa jamii hiyo.
Shambulizi la leo mjini Kabul linatajwa kuwa kubwa kati ya hujuma nyingi zilizoitikisa Afghanistan katika kipindi cha miezi ya hivi karibuni. Takwimu za Wizara ya Afya nchini humo zinasema kuwa, karibu watu 1700 wameuawa katika wimbi la mashambulizi ya kigaidi ndani ya miezi sita ya kwanza ya mwaka huu.
Makundi ya Taleban na Daesh (ISIS) yamekuwa yakihusika na hujuma hizo ambazo weledi wa mambo wanazitaja kuwa, ni njama ya madola ya Magharibi ya kutaka kuendelea kuwepo askari wao nchini humo.
Rais wa zamani wa Afghanistan, Hamid Karzai amelaani shambulizi hilo la mjini Kabul na hujuma nyingine za anga za askari wa Marekani katika mkoa wa Nangarhar ambazo zote zimesababisha mauaji ya makumi ya raia wasio na hatia.