Abbas azidi kuwabinya Wapalestina, akata mitandao ya kijamii
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i32996-abbas_azidi_kuwabinya_wapalestina_akata_mitandao_ya_kijamii
Katika hatua inayoonekana ni ya kuzidi kuwawekea mbinyo Wapalestina, Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina Mahmoud Abbas amepasisha dikrii ya kutaka kufungwa mara moja mitandao ya kijamii na tovuti za habari katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Aug 11, 2017 03:10 UTC
  • Abbas azidi kuwabinya Wapalestina, akata mitandao ya kijamii

Katika hatua inayoonekana ni ya kuzidi kuwawekea mbinyo Wapalestina, Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina Mahmoud Abbas amepasisha dikrii ya kutaka kufungwa mara moja mitandao ya kijamii na tovuti za habari katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan.

Ammar Dweik, Mkuu wa Kamisheni Huru ya Haki za Binadamu ya Palestina amekosoa vikali kitendo hicho na kusema kuwa dikrii hiyo ni moja ya sheria mbaya zaidi zilizowahi kupasishwa tangu Mamlaka ya Ndani ya Palestina ilipoundwa mwaka 1994.

Katika kipindi cha mwezi mmoja, utawala wa Abbas umefunga tovuti 30 za habari, aghalabu yazo zikiwa ni za Mohammed Dahlan, aliyekuwa mpambe wake na zile za Harakati ya Muqawama ya Hamas.

Hivi karibuni, Gazeti la Kizayuni la Haretz liliandika kuwa, Mahmoud Abbas, Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina ni mshirika wa Israel katika kuiwekea mashinikizo Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina (HAMAS) katika Ukanda wa Gaza.

Abbas (Kushoto) na Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu

Siku chache baadaye ikiwa ni katika muendelezo wa hatua za kuwakomoa Wapalestina wa Ukanda wa Gaza, Mahmoud Abbas, Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina aliunda kamati ya usalama kwa lengo la kuwastaafisha kwa nguvu na kabla ya wakati askari elfu moja wa eneo hilo.

Kabla ya uamuzi huo, na katika hatua ya kuzusha mfarakano kwa kisingizio cha kukabiliana na hali mbaya ya kifedha, serikali ya Mamlaka ya Ndani ya Palestina ilichukua uamuzi wa kupunguza mishahara ya wafanyakazi wake katika Ukanda wa Gaza kwa asilimia 30 hadi 50, uamuzi ambao haukuwahusisha wafanyakazi wa mamlaka hiyo katika eneo la Ufukwe wa Magharibi wa Mto Jordan.