Afrika Kusini yasusia kongamno la Kiafrika na utawala haramu wa Kizayuni
Balozi wa Afrika Kusini nchini Lebanon ametangaza kuwa nchi yake imesusia kongamano la viongozi wa Kiafrika na utawala Kizayuni wa lsrael.
Shaun Binfield ameyasema hayo alipokutana na ujumbe wa Sekretarieti ya Watu wa Palestina mjini Bairut, Lebanon na kuongeza kuwa, Afrika Kusini inatambua kikao hicho cha viongozi wa Kiafrika na utawala huo wa Kizayuni kuwa ni hatua yenye lengo la kuboresha mahusiano kati ya lsrael na mataifa ya Afrika na kwa msingi huo, Pretoria imesusia mkutano huo.
Ameongeza kuwa, Afrika Kusini inaendelea kufanya mawasiliano na balozi za mataifa mbalimbali ya Kiafrika na washirika wake ili nazo ziweze kujitenga na utawala huo vamizi wa lsrael. Balozi wa Afrika Kusini nchini Lebanon ameelaani vikali kitendo cha utawala khabithi wa lsrael kuendelea kuuzingira Ukanda wa Gaza na amesisitiza udharura wa kuainishwa njia za kuhitimisha mzingiro huo wa kidhalimu.
Utawala wa Kizayuni wa lsrael ulianzisha mzingiro wa kila upande dhidi ya watu wa Ukanda wa Gaza mwaka 2006, baada ya Harakati ya Muqawama ya Kiislamu ya Palestina (HAMAS) kushinda uchaguzi wa Bunge la Palestina. Tel Aviv inazuia kuingia eneo hilo mafuta, chakula madawa na hata vifaa vya ujenzi.