Aug 25, 2017 07:44 UTC
  • Waislamu milioni 1.4 wameshawasili Saudia kutekeleza Ibada ya Hija

Zaidi ya Waislamu milioni 1.4 wameshawasili Saudi Arabia hadi hivi sasa kwa ajili ya kutekeleza ibada ya kila mwaka ya Hija ambayo inaanza wiki ijayo.

Shirika rasmi la habari la Saudia, SPA, limechapisha ripoti iliyosema hadi kufikia jana Alkhamisi, mahujaji 1,313,946 walikuwa wameshawasili kwa ndege, 79,501 kwa nchi kavu, 12,477 kwa njia ya baharini.”

Idadi hiyo imetajwa kuwa ni ongezeko la asilimia 33 ikilinganishwa na wakati sawa na huo mwaka jana na inatarajiwa kuwa idadi hiyo itapindukiwa milioni mbili.

Ibada ya Hija inatarajiwa kuanza Jumatano ijayo na kuendelea hadi Jumatatu. Mwaka jana idadi kamili ya mahujaji ilikuwa milioni 1.8 ambapo Wairani 64,000 walinyimwa haki yao ya kutekeleza ibada hiyo baada ya Saudi Arabia kukataa kutoa ushirikiano unaohitajika kuwawezesha kusafiri na kuwalindia usalama wao. Tatizo hilo lilitatuliwa mwaka huu baada ya Saudi Arabia kuiomba rasmi Jamhuri ya Kiislamu ya Iran itume mahujaji wake. Iran iliafiki kutuma mahujaji baada ya Saudia kukubali kutekeleza masharti yaliyowekwa na Tehran, hivyo Wairani 86,500 wanatazamiwa kushiriki katika ibada ya Hija mwaka huu.

Mahujaji wakiwa Arafa

Itakumbukuwa kuwa, mwezi Septemba 2015, kulitokea msongamano mkubwa wakati wa ibada ya Hija katika eneo la Mina karibu na Makka ambapo duru zisizo rasmi zinasema mahujaji 7,000 walipoteza maisha huku Saudia ikisisitiza ni watu 770 waliouawa katika msongamano huo. Iran ilitangaza kuwa mahujaji wake wapatao 465 walipoteza maisha katika maafa hayo ya Mina. Siku kadhaa kabla ya tukio hilo, mahujaji 100 walipoteza maisha katika Msikiti Mtakatifu wa Makka, wakiwemo Wairani 11 baada ya winchi kuwaangukia wakati walipokuwa wanatufu al Kaaba.

Maswali mwengi yaliibuka kuhusu uwezo wa Saudi Arabia kusimamia zoezi la Hija ambapo mwaka jana Iran ilitaka usalama wa mahujaji wake udhaminiwe.

 

Tags