Jumuiya kubwa zaidi ya wafanyakazi Canada yasusia Israel
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i33958-jumuiya_kubwa_zaidi_ya_wafanyakazi_canada_yasusia_israel
Jumuiya kubwa zaidi ya wafanyakazi katika sekta binafsi nchini Canada imetangaza rasmi kujiunga na 'Harakati ya Ulimwengu ya Ususiaji wa Israel' maarufu kwa jina la BDS.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Sep 06, 2017 03:41 UTC
  • Jumuiya kubwa zaidi ya wafanyakazi Canada yasusia Israel

Jumuiya kubwa zaidi ya wafanyakazi katika sekta binafsi nchini Canada imetangaza rasmi kujiunga na 'Harakati ya Ulimwengu ya Ususiaji wa Israel' maarufu kwa jina la BDS.

Jumuiya hiyo inayojulikana kwa kifupi kama Unifor hivi karibuni katika kikao chake mjini Winnipeg ilipitisha azimio la kuunga mkono 'Harakati ya Ulimwengu ya Ususiaji Israel' -BDS. Hii ni harakati iliyoanzishwa mwaka 2005 na mashirika kadhaa ya Palestina kwa lengo la kutafuta uungaji mkono wa kimataifa ili kumalizika ukandamizaji unaofanywa na utawala haramu wa Israel dhidi ya Wapalestina na pia kuushinikiza utawala huo uheshimu sheria za kimataifa.

Jumuiya ya Unifor, yenye wanachama zaidi ya 310,000, imesema itaendelea kuunga mkono harakati ya BDS hadi pale utawala wa Kizayuni wa Israel utakapositisha ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu. Unifor pia inataka mamilioni ya Wapalestina waliolazimika kukimbia nchi yao baada ya ardhi zao kunyakuliwa na Israel wawe na haki ya kurejea makwao.

Unifor aidha imetangaza kuunga mkono uundwaji wa nchi huru ya Palestina. Taarifa zinasema utawala wa Kizayuni wa Israel hupata hasara ya takribani dola bilioni 10 kwa mwaka kutokana na ususiwaji unaoongozwa na BDS. Taarifa zinasema Israel imeghadhabishwa sana na uamuzi huo wa wafanyakazi  nchini Canada na kutoa taarifa inayoituhumu Unifor kuwa eti ina chuki dhidi ya Mayahudi.