Sep 14, 2017 14:41 UTC
  • Makumi wakiwemo Wairani 3 wauawa katika miripuko pacha ya mabomu Iraq

Kwa akali watu 50 wakiwemo raia watatu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran wameuawa katika mashambulizi pacha ya mabomu na ufyatuaji risasi huko kusini mwa Iraq.

Jassem al-Khalidi, afisa mwandamizi wa Wizara ya Afya ya Iraq amesema mbali na vifo hivyo, watu wengine karibu 90 wamejeruhiwa katika hujuma hizo za leo Alkhamisi karibu na hoteli moja mjini Nasiriyah, umbali wa kilomita 370 kusini mashariki mwa mji mkuu Baghdad, katika mkoa wa Dhi Qar ulioko kusini mwa nchi.

Saad Maan, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Iraq naye amesema mbali na mkusanyiko mkubwa watu waliokuwa ndani na nje ya hoteli hiyo karibu na kituo cha upekuzi kufariki dunia katika miripuko pacha, wengine miongoni mwao wamepoteza maisha baada ya kufyatuliwa risasi.

Sehemu moja iliyoharibiwa na miripuko ya mabomu nchini Iraq

Hadi tunaenda mitamboni, hakuna kundi lolote lilikuwa limetangaza kufanya mashambulizi hayo ingawaje dalili zote zinaashiria kuwa yametekelezwa na kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh.

Haya yanajiri siku chache baada ya mji wa Tal Afar wa magharibi mwa mkoa wa Nainawa (Nineve) huko kaskazini mwa Iraq kukombolewa katika operesheni ya kuwafurusha magaidi wa ISIS mjini humo.

Kwa mujibu wa Timu ya Utoaji Misaada ya Umoja wa Mataifa nchini Iraq (UNAMI), raia zaidi ya 125 wameuawa huku wengine karibu 200 wakijeruhiwa katika wimbi la hujuma za kigaidi za Daesh ndani ya mwezi uliopita pekee wa Agosti.

Tags