Brigedi ya Izzudeen Qassam yatangaza himaya yake kwa Waislamu wa Myanmar
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i34437-brigedi_ya_izzudeen_qassam_yatangaza_himaya_yake_kwa_waislamu_wa_myanmar
Brigedi ya Izzudeen Qassam tawi la kijeshi la Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS imefanya gwaride kubwa kama ishara ya kufungmana na wananchi Waislamu wa Myanmar wanaokabiliwa na unyama na ukatili wa mabudha wanaosaidiwa na jeshi la nchi hiyo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Sep 16, 2017 09:17 UTC
  • Brigedi ya Izzudeen Qassam yatangaza himaya yake kwa Waislamu wa Myanmar

Brigedi ya Izzudeen Qassam tawi la kijeshi la Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS imefanya gwaride kubwa kama ishara ya kufungmana na wananchi Waislamu wa Myanmar wanaokabiliwa na unyama na ukatili wa mabudha wanaosaidiwa na jeshi la nchi hiyo.

Wanapambano wa tawi hilo la kijeshi la Hamas waliokuwa wakifanya gwaride lao katika mitaa ya mji wa Khan Yunis katika Ukanda wa Gaza wakiwa wamebeba mabango yenye jumbe mbalimbali wamelaani vikali jinai za jeshi la Myanmar dhidi ya Waislamu wa Rohingya.

Maafisa wa Brigedi ya Izzudeen Qassam tawi la kijeshi la Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS wametoa wito kwa jamii ya kimataifa kuchukua hatua za haraka kusitisha jinai dhidi ya Waislamu wa Rohingya.

Aidha taarifa ya viongozi hao imeeleza kwamba, kile kinachofanywa dhidi ya Waislamu wa Rohingya ni jinai dhidi ya binadamu.

Maelfu ya nyumba za Waislamu wa Rohingya zimechomwa moto katika jimbo la Rakhine

Umoja wa Mataifa umetangaza kuwa, zaidi ya Waislamu laki nne wa Rohingya wamelazimishwa kuhama makazi yao na kukimbilia Bangladesh tangu tarehe 25 mwezi uliopita wa Agosti kutokana na ukatili na mauaji yanayofanywa na Mabudha. Waislamu wengine zaidi ya elfu sita wameuawa na wengine elfu 8 wamejeruhiwa. 

Ukatili mkubwa zaidi dhidi ya Waislamu nchini Myanmar unafanyika katika mkoa wa Rakhine ulioko magharibi mwa nchi hiyo. 

Wakati huo huo, maandamano ya kulaani jinai dhidi ya Waislamu wa Myanmar yameendelea kushuhudiwa katika pembe mbalimbali ulimwenguni huku Umoja wa Mataifa na Baraza la Usalama zikitakiwa kuchukua hatua ili kukomesha maafa na jinai dhidi ya Waislamu hao.