Sep 22, 2017 12:25 UTC
  • Muharram; mwezi wa rehema na huruma

Mwezi wa Muharram ni mwezi wa rehema na huruma na ambao unaweza kuyafanya makundi na madhehebu tofauti ya Kiislamu kuwa na uhusiano mzuri wa kimaanawi.

Pamoja na hayo kuna makundi maovu ambayo yameazimia kuleta mgawanyiko na hitilafu miongoni mwa jamii ya Waislamu kwa kuendesha mauaji ya kutisha dhidi yao. Mlipuko wa kigaidi uliotekelezwa katika mwezi wa Muharram nchini Saudi Arabia mwaka 2015 ni mfano wa wazi kuhusiana na suala hilo. Mwaka 2015 kudi la kigaidi la Daesh lilitoa taarifa likitangaza kuhusiana na tukio hilo la kigaidi dhidi ya Mashia wa Saudi Arabia. Kundi hilo limehusika na matukio mengi kama hayo nchini humo. Mwezi Mei mwaka 2014 magaidi wa kundi hilo la kitakfiri walivamia msikiti mmoja wa Mashia katika mji wa Dammam na kuwaua kinyama watu wanne waliokuwa wakitekeleza ibada zao kwenye msikiti huo. Katika tukio jingine kama hilo katika mji wa Qadeeh ulio karibu na mji wa Qatif magaidi hao walifanya shambulio jingine la kinyama na kuwaua Mashia 24 wasio na hatia. Kabla ya hapo Shirika la Msamaha Duniani, Amnesty International, lilikuwa limeutaka utawala wa Saudia kuchukua hatua za lazima kwa ajili ya kuwalinda Mashia waliowachache nchini humo kutokana na mashambulio ya mara kwa mara ya magaidi wa Daesh, likisema kuwa mashambulio kama hayo dhidi ya misikiti ya Mashia yalikuwa yameongezeka kwa kiwango cha kutisha.

Mashia wa Saudia wakifanya maandamano dhidi ya mauaji na ukandamiza wa utawala wa nchi hiyo

Jambo la kushangaza ni kuwa mashambulio kama hayo ya kigaidi yamekuwa yakiripotiwa katika maeneo ambayo Waislamu wa madhebu tofauti ya Kiislamu wamekuwa wakiishi pamoja kwa amani, maelewano na ushirikiano. Matukio kama hayo pia yamekuwa yakiripotiwa kwa wingi katika maeneo tofauti ya Pakistan na hasa katika mwezi kama huu mtukufu wa Muharram. Kuhusiana na suala hilo, Majid Hairani, mwandishi wa shirika la habari la Sky News anasema: ''Daima Pakistan imekuwa ikikabiliwa na changamoto katika mwezi wa kwanza wa Hijiria. Mwaka 2013 ndugu wawili wa Kisuni Sami' ad-Deen na Swalah ad-Deen wakazi wa Pishawar ambao waliamua kushiriki katika maombolezo ya Muharram mjini humo waliuawa. Magaidi ambao hawakuvumilia kuona ishara hiyo ya udugu na umoja kati ya Waislamu, waliamua kuwaua ndugu wawili hao kwa kuwafyatulia risasi. Vilevile mwaka 2012 Mawahabi waliua waombolezaji 28 na kuwajeruhi wengine 70 katika maombolezo ya Muharram kupitia shambulio la kujilipua kwa bomu. mwaka 2013 kundi jingine la kigaidi la Taliban la nchini Pakistan lilitangaza kuhusika na milipuko hiyo ya kufuatana iliyotokea katika Husseinia na mikusanyiko ya waombolezaji wa Kishia katika miji ya Karachi na Rawalpindi. Allama Rajah Nassir Katibu Mkuu wa chama cha Majlisi ya Umoja wa Waislamu wa Pakistan na  pia Altaf Hussein, Mkuu wa Harakati ya Kitaifa ya Umoja ya Pakistan walilaani vikali mashambulio hayo na kuitaka serikali iwadhaminie waombolezaji usalama.'' Mwisho wa kunukuu.

Moja ya milipuko ya kigaidi Pakistan

Mwezi wa Muharram kwa Waislamu ni mwezi wa mapambano pia. Ni kutokana na ukweli huo ndipo tawala vibaraka zikahofia mkusanyiko mdogo tu wa waomboleza wa mjuu wa Mtume Mtukufu (saw). Huu ndio ndio ukweli mchungu unaowakabili pia wananchi wa Bharain. Is'haq Anjazi, mtaalamu wa masuala ya kisiasa anasema: 'Kwa mara nyingine tena watu wa Bahrain wameonyesha hasira zao kuhusiana na uvunnjiwaji heshima maombolezo ya siku za Muharram unaofanywa na utawala wa nchi hiyo, kwa kufanya maandamano dhidi ya utawala wa Aal Khalifa. Askari usalama wa utawala huo wamekusanya mabango na maberamu yote yanayohusiana na maombolezo ya Muharram. Utawala wa Aal Khalifa tokea mwaka 2011 hadi sasa umekuwa ukikandamiza vikali malalamiko na maandamano ya wapinzani na kubana kabisa shughuli zao za kijamii. Utawala huo pia kufikia sasa umeua makumi ya wapinzani na kufunga jela mamia ya wegine.'' Mwisho wa kunukuu.

Ama ni kwa nini wapinzani wa maombolezo hayo ya kidini huingiwa na hofu na uoga kila yanapofanyika? Ni wazi kuwa nguvu na nishati inayotokana na Muharram kwa  ajili ya kuwaunganisha Waislamu daima huwatia hofu wapinzani na hivyo kutaka mwenendo wake ubadilishwe.

Maandamano ya Mashia wa Bahrain dhidi ya ukandamizaji wa serikali

Kuhusu hilo Adnan Sawajiri, mwanaharakati wa kisiasa anasema: ''Suala la kuwepo madhahebu tofauti ni jambo linalokubalika katika Uislamu. Pamoja na hayo, kuna makundi ambayo daima yanataka kuzua hitilafu miongoni mwa Waislamu ili yapate kuendeleza siasa zao. Kitambo ni wakoloni wa Uingereza na Ufaransa ndio waliokuwa wakiwasha moto wa hitilafu hizo lakini hivi sasa ni makundi ya kitakfiri ndiyo yanayoua Waislamu wa Shia na Suni kwa jina la 'Mwenyezi Mungu'." Kuna itikadi mpya ambayo imejitokeza katika kipindi cha karne moja iliyopita ambayo inakufurisha wengine kirahisi kabisa na kuua Waislamu wenzao. Bila shaka mshindi wa mchezo huo hatari ni nchi za kibeberu na maadui wa Uislamu." Mwisho wa nukuu.

Pamoja na hayo, sasa watu wote wanafahamu kwamba Muharram ni harakati ya kisiasa na kidini iliyo na lengo maalumu la kudhihirisha uwezo na nguvu ya Kiislamu, ambayo licha ya kukabiliwa na vitendo vya ugaidi wa kujilipua kwa mabomu, lakini vitendo hivyo vimeshindwa kabisa kupunguza matokeo yake chanya ya kuleta umoja na mshikamano kati ya Mashia na Masuni.

Tags