Rais al-Assad: Mataifa ya Kiarabu yanaliunga mkono taifa la Syria
(last modified Sun, 24 Sep 2017 03:32:29 GMT )
Sep 24, 2017 03:32 UTC
  • Rais al-Assad: Mataifa ya Kiarabu yanaliunga mkono taifa la Syria

Rais Bashar al-Assad wa Syria amesema kuwa, akthari ya mataifa ya Kiarabu yanaliunga mkono taifa la Syria, lakini tawala za Warabu zinawaunga mkono magaidi wanaopigana dhidi ya serikali ya Damascus.

Hata hivyo Rais wa Syria amesisitiza kuwa, uungaji mkono huo wa tawala za Kiarabu kwa magaidi hauwezi kuwa na taathira.

Rais al-Assad ameyasema hayo alipokutana na ujumbe wa Bunge la Mauritania unaoongozwa na Mohamed Ould Vall, kiongozi wa chama cha 'Ustawi' cha nchi hiyo na kusisitiza kuwa, safari za jumbe za wananchi kutoka mataifa mbalimbali ya Kiarabu nchini Syria zina ujumbe maalumu na mkubwa kwa taifa la Syria.

Rais Bashar al-Assad akizungumza na ujumbe huo

Ameongeza kuwa suala hilo linaonesha kuwa mataifa mengi ya Kiarabu yamesimama bega kwa bega na Wasyria. Rais Bashar al-Assad amesema kuwa, mazungumzo hususan kati ya mabunge na vyama tofauti katika uga wa Kiarabu, ni suala la msingi kwa ajili ya kukurubisha pamoja mitazamo mbalimbali ili kuweza kukabiliana na changamoto zinazoyakabili mataifa ya Kiarabu. 

Raia wa Syria wakionyesha uungaji mkono wao kwa Rais Bashar al-Assad katika uchaguzi

Kwa upande wake ujumbe wa Bunge la Mauritani katika kikao hicho umesema kuwa, msimamo rasmi wa wananchi na raia wa Mauritania ni kuunga mkono raia wa Syria, jeshi na viongozi wa serikali ambao wanakabiliwa na mashambulizi ambayo hayajawahi kushuhudiwa ya kigaidi. Ujumbe huo umesisitiza kuwa, ushindi wa serikali ya Damascus dhidi ya magaidi sio ushindi wa Wasyria pekee, bali ni kwa ajili ya wapigania uhuru wote wa dunia.

Sehemu nyingine ujumbe huo imesema kuwa, kuna matumaini kwamba, kusimama imara raia wa Syria kwa kipindi cha miaka kadhaa iliyopita kunaweza kwa mara nyingine kuwa msingi wa ujenzi mpya wa taifa lao.