Hamas yalaani ukatili unaofanywa na Wazayuni
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i3481-hamas_yalaani_ukatili_unaofanywa_na_wazayuni
Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina Hamas imelaani vikali hatua ya Wazayuni wa Israel ya kuchoma moto nyumba ya shahidi pekee wa jinai ya kuchomwa moto nyumba na familia ya al Sa'ad Dawabsheh na kuteketezwa watu wa familia hiyo wakiwa hai.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Mar 20, 2016 22:48 UTC
  • Hamas yalaani ukatili unaofanywa na Wazayuni

Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina Hamas imelaani vikali hatua ya Wazayuni wa Israel ya kuchoma moto nyumba ya shahidi pekee wa jinai ya kuchomwa moto nyumba na familia ya al Sa'ad Dawabsheh na kuteketezwa watu wa familia hiyo wakiwa hai.

Izzat Rashaq ambaye ni mwanachama wa Idara ya Siasa ya harakati ya Hamas amesema kuwa, kuchomwa moto nyumba ya shahidi pekee wa uhalifu na jinai ya kuchomwa moto nyumba ya familia ya Sa'ad Dawabsheh katika kijiji cha Duma huko katika Ukingo wa Magharibi hakuwezi kuficha ukatili na unyama wa walowezi wa Kizayuni. Izzat Rashaq amekosoa kimya cha jamii ya kimataifa kuhusu jinai za Israel huko Palestina na kusema viongozi wa utawala huo ghasibu wanaendelea kufanya uhalifu wa kutisha dhidi ya raia wa Palestina bila ya kuchukuliwa hatua yoyote.

Wakati huo huo Jumuiya ya Nchi za Kiarabu imelaani jinai ya walowezi wa Kizayuni katika kijiji cha Duma. Naibu Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu, Said Abu Ali ametoa wito wa kukabiliana na jinai zinaofanywa na Wazayuni katika ardhi za Palestina.

Wazayuni wenye misimamo mikali waliokuwa wakisaidiwa na kupewa himaya na askari wa Israel jana Jumapili walivamia na kuchoma moto nyumba ya shahidi pekee wa jinai ya kuchomwa moto nyumba ya familia ya Sa'ad Dawabsheh huko Ukingo wa Magharibi.

Miezi kadhaa iliyopita walowezi wa Kiyahudi walichoma moto nyumba ya familia ya Sa'ad Dawabsheh na kumuua shahidi yeye, mke na mtoto wake mdogo aliyekuwa na umri wa miezi 18.