Wapalestina: Uingereza iliombe radhi taifa la Palestina kwa Azimio la Balfour
Wakati serikali ya Uingereza inatazamiwa kusherehekea maadhimisho ya miaka 100 tangu kutolewa Azimio la Balfour, makundi ya Kipalestina yamesisitizia ulazima wa serikali ya London kuliomba radhi taifa la Palestina kwa sababu ya kutoa azimio hilo.
Katika Azimio la Balfour la mwaka 1917, Waziri wa Mambo ya Nje wa wakati huo wa Uingereza Arthur James Balfour, alimwandikia barua ya kumtaarifu Walter Rothschild, mwanasiasa wa Kizayuni na mbunge wa bunge la Uingereza kuhusu mtazamo chanya wa serikali ya London juu ya "kuanzishwa nyumba ya kitaifa kwa ajili ya Waisraeli katika ardhi ya Palestina".
Azimio hilo la Balfour lilikuwa ndiyo cheche na mwanzo wa njama na fitna ya kuasisiwa utawala haramu wa Kizayuni wa Israel katika ardhi za Palestina.
Jana Jumatano, makundi ya kitaifa na Kiislamu ya Palestina yaliandamana na kukusanyika mbele ya jengo la Baraza la Kiutamaduni la Uingereza linalotambulika kama nembo ya nchi hiyo ndani ya ardhi ya Palestina huko mjini Ramallah, Ufukwe wa Magharibi wa Mto Jordan na kusisitiza ulazima wa serikali ya Uingereza kufuta mpango wa kufanya sherehe za kuadhimisha kutimia miaka 100 tangu kutangazwa azimio hilo.
Isam Bakr, mratibu wa makundi ya kitaifa na Kiislamu ya Palestina katika miji ya Ramallah na Albirah alitangaza pembeni ya mjumuiko huo kwamba Uingereza ina wajibu wa kufidia dhulma ya kihistoria iliyolifanyia taifa la Palestina.
Bakr aidha ameitaka Jamii ya Kimataifa ichukue hatua za kukomesha jinai za kibaguzi za utawala wa Israel dhidi ya Wapalestina pamoja na kuuchukulia hatua utawala huo na kuushinikiza uheshimu sheria za kimataifa.../