UNICEF: Mzingiro wa Saudia utaua maelfu ya watoto Wayemen wenye njaa
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i36305-unicef_mzingiro_wa_saudia_utaua_maelfu_ya_watoto_wayemen_wenye_njaa
Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuwahudumia Watoto UNICEF limeonya kuhusu madhara makubwa ya mzingiro wa Saudi Arabia dhidi ya Yemen na kusema idadi kubwa ya watoto Wayemen wanaweza kupoteza maisha kwani tayari wanakabiliwa na lishe duni.
(last modified 2024-06-10T09:25:34+00:00 )
Nov 10, 2017 15:08 UTC
  • UNICEF: Mzingiro wa Saudia utaua maelfu ya watoto Wayemen wenye njaa

Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuwahudumia Watoto UNICEF limeonya kuhusu madhara makubwa ya mzingiro wa Saudi Arabia dhidi ya Yemen na kusema idadi kubwa ya watoto Wayemen wanaweza kupoteza maisha kwani tayari wanakabiliwa na lishe duni.

Katika taarifa, Mkurugenzi Mtendaji wa UNICEF Anthony Lake ameonya kuwa,  hatua ya Saudia kufunga viwanja vyote vya ndege na bandari zote Yemen ni jambo ambalo limeyafanya maafa ya nchi hiyo inayokumbwa na vita kuwa mabaya zaidi.

Mapema wiki hii jeshi la Saudia lilishadidisha mzingiro dhidi ya Yemen kwa kufunga njia zote za ndege na meli na kuzuia misaada ya kibinadamu kuingia nchini humo baada ya Jeshi la Yemen kuvurumisha kombora lililotua katika uwanja wa ndege ya Riyadh katika hatua ya kulipiza kisasi.

Mzingiro wa Yemen uliwekwa mwezi Machi mwaka 2015 wakati Saudi Arabia na waitifaki wake walipoanzisha hujuma ya kinyama na haramu dhidi ya taifa la Yemen.

Watoto ni waathirika wakubwa wa hujuma za Saudia kila siku dhidi ya taifa la Yemen

UNICEF imesema hivi sasa watoto 400,000 nchini Yemen wanakabiliwa na hatari ya kifo kutokana na kiwango kikubwa cha lishe duni na kuwa mzingiro huo wa Saudia utapelekea idadi hiyo kuongezeka na kwamba kuna uwezekano wa watoto wengi kupoteza maisha.

Hayo yanajiri wakati ambao Msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ameeleza wasiwasi wake kuhusu hatua ya Saudi Arabia na washirika wake ya kufunga kabisa mipaka ya Yemen kwa siku ya tano mfululizo na kusisitiza kuwa Yemen inakabiliwa na baa kubwa zaidi la njaa duniani.