Msimamo wa undumakuwili wa Ufaransa kuhusiana na Saudi Arabia
(last modified Fri, 01 Dec 2017 07:21:37 GMT )
Dec 01, 2017 07:21 UTC
  • Msimamo wa undumakuwili wa Ufaransa kuhusiana na Saudi Arabia

Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa alitangaza siku ya Jumatano kuwa Saudi Arabia inapaswa ikatishe ufadhili wake wa kifedha kwa makundi ya kigaidi katika eneo la Mashariki ya Kati.

Macron alisisitiza kwamba Paris itawapatia viongozi wa utawala wa Aal Saud orodha ya majina ya makundi ya kigaidi ili Riyadh ikatishe kuyasaidia kifedha makundi hayo.

Msimamo huo uliotangazwa na rais wa Ufaransa kuhusiana na utawala wa Saudia unaweka wazi kwa mara nyengine tena sera za migongano za Paris, iwe ni katika uhusiano wake na Saudi Arabia au katika uchukuaji hatua za kindumakuwili katika suala la kupambana na ugaidi.

Ufaransa ina uhusiano mkubwa na Saudi Arabia na wakati huohuo inataka kustawisha na kupanua zaidi uhusiano wake huo na Riyadh. Hata hivyo Macron mwenyewe amekiri kwamba utawala wa Aal Saud ni miongoni mwa wafadhili wa kifedha wa makundi ya kigaidi, na ametaka kukatishwa ufadhili huo kwa makundi hayo. Pamoja na hayo inafaa tuseme kwamba msimamo wa ukosoaji wa rais wa Ufaransa kwa Riyadh ni hila tu ya kutaka kuwahadaa watu wa kawaida.

Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa (kushoto) alipokutana na mrithi wa Ufalme wa Saudia mjini Riyadh

Ni kama alivyosema Laurence Nado, mtaalamu wa taasisi ya uhusiano wa kimataifa ya Ufaransa, kwamba ugaidi ambao dunia inakabiliana nao hivi sasa hauungwi mkono na Iran, bali unafadhiliwa zaidi na wafalme wa nchi za pembezoni mwa Ghuba ya Uajemi.

Suali la kujiuliza sasa ni kwamba, ikiwa Ufaransa inaitakidi kuwa, yenyewe ni miongoni mwa waathiriwa wa mashambulio ya kigaidi; na kwa kisingizio hicho, baada ya mashambulio ya kigaidi ya mwaka 2016 ya mjini Paris ilianzisha operesheni za mashambulio dhidi ya magaidi kupitia muungano wa kimataifa wa eti kupambana na Daesh, vipi inakuwa na uhusiano wa karibu na mmoja wa wafadhili na waungaji mkono wakubwa wa kifedha wa makundi ya kigaidi? Jibu la suali hili linapatikana kwa kuyachambua maslahi na manufaa makubwa inayopata Paris katika uhusiano wa karibu uliopo baina yake na utawala wa Riyadh.

Katika masuala mbalimbali ya eneo la Mashariki ya Kati, siku zote Ufaransa imekuwa ikichukua msimamo unaokaribiana na ule wa Saudia. Na sababu ya jambo hilo iko wazi. Kwa kuzingatia kwamba Saudi Arabia ni mmoja wa wasafirishaji wakubwa wa mafuta duniani na wakati huohuo ni mmoja wa wanunuzi wakubwa zaidi wa silaha ulimwenguni, kila pale viongozi wa Paris wanapofanya safari nchini Saudia hujitahidi kuonyesha kwamba misimamo na mielekeo yao inakaribiana na ya watawala wa Riyadh ili kuweza kuandaa mazingira ya kufunga mikataba na nchi hiyo, yenye faida nono za kibiashara na kiuchumi pamoja na ya kijeshi.

Chati inayoonyesha Ufaransa ikiongoza kwa mauzo ya silaha kwa Saudia miongoni mwa nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya

Katika safari ya karibuni pia aliyofanya Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa mjini Riyadh, kiongozi huyo alionyesha misimamo ya upinzani dhidi ya Iran hususan kuhusu mpango wa makombora wa Tehran na shambulio la kombora la Yemen dhidi ya Saudia, hatua ambayo imetafsiriwa kuwa ni kutumia Paris mivutano iliyopo katika eneo hili kwa manufaa yake. Na bila ya shaka ujanja huo wa serikali ya Ufaransa wa kucheza na kufuata mdundo wa ngoma inayopigwa na utawala wa Aal Saud umekuwa na matunda na faida kubwa za kiuchumi kwa Paris, maana uliandamana na kusainiwa na pande mbili mikataba ya kibiashara na ya uuzaji silaha yenye faida kubwa kwa Ufaransa.

Viongozi wa Ufaransa wana matumaini kwamba kwa kusaini mikataba hiyo ya kiviwanda na kijeshi na Saudia wataweza kustawisha uchumi wa nchi yao na kupunguza idadi ya Wafaransa wasio na ajira. Ukweli ni kwamba viongizi wa Ikulu ya Élysée wanaielewa fika nafasi haribifu ya utawala wa Aal Saud katika kueneza na kushamirisha ugaidi katika Mashariki ya Kati, hususan katika nchi za Syria na Iraq; na kimsingi Ufaransa yenyewe ilikuwa miongoni mwa waungaji mkono wa makundi hayo ya kigaidi. Kwa kweli moja ya sababu muhimu zaidi za kuenea ugaidi ni kukabiliana nao kinafiki na kindumakuwili kunakofanywa na Wamagharibi, Ufaransa ikiwa miongoni mwao.

Peter Neumann, mtaalamu wa kijerumani, anaashiria jinsi kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh (ISIS) lilivyoundwa na kupata nguvu na kusema: "matokeo hasi ya kile kilichotokea nchini Syria yataendelea kutuandama kwa miaka mingi ijayo." Kwa muktadha huo inapasa tusisitize tena kwamba msimamo uliotangazwa na rais wa Ufaransa ni hila tu ya kujaribu kuwahadaa watu wa kawaida na kutaka kuonyesha ndani ya Ufaransa na katika uga wa kimataifa kwamba msimamo wa Paris ni wa kupiga vita ugaidi.../