Wajordan waandamana kumlaani Rais wa Marekani
Wananchi wa Jordan pamoja na viongozi wa sekta mbalimbali akiwemo spika wa bunge la nchi hiyo wamefanya maandamano karibu na ubalozi wa Marekani mjini Amman kulaani hatua ya rais wa Marekani, Donald Trump, ya kuitambua Baytul Muqaddas kuwa mji mkuu wa utawala ghasibu wa Kizayuni.
Maandamano ya wapenda haki yameenea katika kila kona ya dunia kulaani kitendo cha Trump cha kupotosha historia na kudai kuwa eti Quds ni mji mkuu wa Israel.
Waandamanaji hao wamebeba bendera za Palestina na za Jordan na kuwalaani Muhammad bin Salman, mrithi wa kiti cha ufalme wa Saudia na Donald Trump wa Marekani kwa kitendo hicho cha kuwachochea Waislamu.
Hii ni mara ya kwanza kwa wananchi wa Jordan kutoa nara na kaulimbiu za kuwalaani viongozi wa Saudi Arabia ambao wanaonekana kuunga mkono tangazo hilo la rais wa Marekani dhidi ya mji mtakatifu wa Quds wenye Kibla cha Kwanza cha Waislamu.
Hata hivyo hasira kubwa zaidi za waandamanaji hao zimeelekezwa kwa Donald Trump ambaye wamemwita punguwani, mwendawazimu na majivuno.
Jana Ijumaa pia wananchi wa kona zote za Iran walifanya maandamano kulaani uadui wa rais wa Marekani na kusisitiza kuwa kuna siku Wazayuni watafurushwa katika kila shibri ya ardhi za Palestina.
Viongozi wa nchi mbalimbali duniani nao wamelaani hatua hiyo wakiwemo wa Ulaya kama Uingereza na Papa Francis, kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani.
Naye Kim Jong-un, Kiongozi wa Korea Kaskazini ameubeza uamuzi wa Rais wa Marekani wa kuitangaza Quds kuwa mji mkuu wa Israel na kusema kuwa, hakuna nchi inayojulikana kwa jina la Israel hata Baitul Muqaddas uwe mji mkuu wake.