Kuchanganyikiwa Trump katika sera zake kuhusiana na Mashariki ya Kati
Siasa na sera za Marekani katika Mashariki ya Kati siku zote zimekuwa kwa namna fulani zikiandamana na nia mbaya na malengo maovu. Na zaidi katika miaka ya karibuni ambapo, Marekani haijapata matunda yoyote ya maana katika eneo hili zaidi ya kuzusha mivutano, vitisho, machafuko na kuvuruga hali ya mambo. Na hii ni pamoja na kwamba marais wote wanaokuja na kuondoka nchini Marekani husema kuwa wanataka kurasimisha demokrasia katika eneo hili muhimu.
Lakini kile kinachodhihirisha suala hilo kwa uwazi zaidi hivi sasa kuliko ilivyokuwa hapo kabla ni matamshi ya rais mpya wa Marekani ambaye anakiri waziwazi kuhusu siasa na sera za nchi hiyo katika Mashariki ya Kati. Anachofanya Trump, ama kinatokana na mpango ulioratibiwa tokea hapo kabla au ni kwa sababu ya kutokuwa na tajiriba yoyote katika uga wa kisiasa. Mfano hai wa hilo ni sera za Washington kuhusiana na Saudi Arabia ambayo ameifananisha na ng'ombe wa maziwa anayepasa kukamuliwa hadi tone lake la mwisho; na baada ya kukaukwa na maziwa yote ni kumchinja na kula nyama yake. Na hivi hivi ndivyo zilivyokuwa sera za miaka ya nyuma za Marekani katika Mashariki ya Kati.
Nukta ya kuvutia hapa ni kuwa hivi sasa hata vyombo vya habari vya ndani ya Marekani navyo pia vimekiri kuwa pamoja na majigambo yake yote, si serikali wala si Trump mwenyewe ambaye ana sera maalumu na mkakati sahihi anaoutumia katika Mashariki ya Kati zaidi ya kushughulishwa na jinsi ya kulinda na kufanikisha maslahi ya Marekani tu katika eneo hili.
Makala moja ya hivi karibuni ya gazeti la Washington Post imetilia mkazo nukta hiihii na kueleza kwamba Trump hana sera yoyote kuhusiana na Mashariki ya Kati.
Baada ya miezi 11 tangu kuanza urais wa Donald Trump, sera za nje za Marekani zimekuwa zikikwaa visiki mbalimbali ikiwemo hatua ya Washington ya kujichukulia hatua ya upande mmoja ya kuishambulia kijeshi Syria, kukataa kuthibitisha kuwa Iran imetekeleza kikamilifu makubaliano ya nyuklia na kuitambua Quds tukufu kuwa mji mkuu wa Israel. Matokeo ya siasa hizo ghalati za Marekani yamekuwa ni kujitokeza miungano mipya dhidi ya nchi hiyo katika eneo na tab'an kushuka mno kiwango cha uaminifu na itibari ya Marekani mbele ya nchi muhimu duniani zikiwemo hata waitifaki wa Washington.

Hatua ya upande mmoja ya kuishambulia Syria kwa kisingizio cha kutumia silaha za kemikali na kukataa kuthibitisha kufungamana Iran na makubaliano ya JCPOA kwa matumaini kwamba Umoja wa Ulaya na Kongresi ya Marekani zitachukua hatua dhidi ya Iran ndizo sera muhimu zaidi zilizofuatwa na Washington katika muda huu wa mwaka mmoja katika Mashariki ya Kati, ambapo tangazo la kuitambua rasmi Baitul Muqaddas kuwa mji mkuu wa Israel - katika hali ambayo Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani amesema itapita miaka kadhaa kabla ya ubalozi wa Marekani kuhamishiwa kwenye mji huo - limezidi kudhihirisha hali ya mkanganyo na kukosekana uwiyano katika sera hizo za Washington.
Kwa mtazamo wa gazeti la Washington Post: sera hizi za nje za serikali ya Trump zimesababisha mkengeuko, kuvurugika uthabiti na kujitokeza muungano wa Russia na Iran na si wa Marekani na Israel katika Mashariki ya Kati.
Eric Edelman, balozi wa zamani wa Marekani nchini Uturuki aliwasilisha ripoti maalumu mbele ya kamati ya vikosi vya ulinzi ya Baraza la Seneti akawaeleza hivi maseneta wa Marekani kuhusu sera na siasa za Trump:
"Sera za Donald Trump katika eneo mpaka wakati huu, japokuwa zimetegemea mno utoaji maneno mengi, lakini kiuhalisia ni muendelezo wa sera zilezile za marais waliopita wa Marekani".
Wataalamu wengi wa siasa wametahadharisha kuwa leo hii kuna vitisho viwili vikuu na vinavyokinzana ambavyo vinatishia maslahi ya Marekani katika Mashariki ya Kati. Cha kwanza ni Iran ambayo nguvu zake katika eneo zinazidi kuongezeka; lakini pia ni makundi yenye misimamo ya kufurutu mpaka ambayo kutokana na misaada ya mbali na karibu ya Marekani kwa makundi hayo yamesababisha migogoro na maafa mengi na makubwa katika eneo. Hata hivyo Trump, akiwa ni rais wa Marekani amekosa kuwa na ufahamu wa kutosha wa hatari hizo; na wataalamu hao wameshindwa kumshawishi akubaliane na mtazamo wa kuchukua hatua za haraka na za dharura kuhusiana na hali ya eneo.
Kwa kumalizia inapasa tuseme kuwa sera za nje za Donald Trump zitazidisha mivutano na hata kuzuka vita vikubwa katika eneo. Sera hizo zinalenga kuzitumia nchi zinazopinga kuwa na nguvu Iran ili kudhibiti ushawishi na satua ya Iran kwa njia ya kuzifanya nchi hizo pia zijiingize moja kwa moja kijeshi na katika vikwazo vya kiuchumi na teknolojia dhidi ya Iran. Katika hali kama hiyo amani hata ya kiwango kidogo ya Mashariki ya Kati itakumbwa na migogoro mikubwa ambapo kosa lolote la kistratijia litakalofanywa na nchi husika linaweza kusababisha kutokea vita vya eneo zima katika Mashariki ya Kati. Kutangazwa Quds kuwa mji mkuu wa utawala wa Kizayuni kumeifanya hali hiyo ya mambo iwe tata zaidi kuliko ilivyofikiria timu ya Trump.../