Kutaja jina la Jumuiya ya Nchi za Kiarabu kunatia kichefuchefu
Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Saudi Arabia amedai katika maneno ya kuchekesha na kustaajabisha kwa wakati mmoja kwamba, nchi hiyo na utawala wa Kizayuni wa Israel hazina uhusiano rasmi lakini Riyadh ina ramani ya njia eti ya mpango wa Kiarabu wa kuanzisha uhusiano wa kawaida na Tel Aviv.
Matamshi hayo yametolewa karibu mwezi mmoja baada ya waziri wa serikali ya Israel kutangaza kuwa, utawala huo na Saudi Arabia zina uhusiano na wasiwasi wa pamoja kuhusu Iran.
Iran ni adui wa pamoja wa Israel na utawala wa kifalme wa Saudi Arabia kwa mujibu wa methali maarufu inayosema: Adui wa adui yangu ni rafiki yangu. Maafisa wa pande hizo mbili wamekuwa wakikutana mara kwa mara na kueneza propaganda chafu dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu. Japokuwa hadi sasa hakuna uhusiano wa wazi na rasmi baina ya Saudi Arabia na Israel, lakini kwa hakika pande hizo zimekuwa zikishirikiana katika mambo mengi. Hata hivyo katika siku za hivi karibuni mikutana na mahusiano ya Saudia na Israel yamenza kuonekana waziwazi na Waziri wa Nishati wa serikali ya Tel Aviv, Yuval Steinitz alikuwa afisa wa kwanza rasmi wa utawala huo kufichua wazi uhusiano uliopo baina ya watawala wa Aal Saud na serikali ya Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu. Kwa upande wao, watawala wa Saudi Arabia wangani na woga wa kutangaza rasmi uhusiano wao na utawala ambao umevamia na kukalia kwa mabavu Kibla cha Kwanza cha Waislamu. Ni wazi kuwa, nafasi na mchango wa Iran wa kufichua njama za mabeberu na vibaraka wao umezifanya tawala hizo mbili zikaribiane zaidi.
Inasikitisha kumsikia Adel Al Jubeir Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Saudi Arabia, nchi inayojinadi kuwa ni Ummul Quraa na kitovu cha ulimwengu wa Kiislamu, na mfalme wake akidai kuwa "mtumishi wa Haram mbili za Makka na Madina", akisema tena kwa kujigamba kwamba: Iwapo kutapatikana amani baina ya Palestina na utawala unaoikaliwa Quds kwa mabavu, Riyadh itaanzisha uhusiano wa kiuchumi, kibiashara na kisiasa na Israel bila ya aibu yoyote! Naam bila ya aibu yoyote!!
Mtafiti wa Taasisi ta Ghuba ya Uajemi, Hussein Aibish anasema: Matamshi ya Waziri wa Nishati wa Israel hayaushangazi ulimwengu wa Kiarabu, hii ni kwa sababu watu wote wanajua kuwa pande hizo mbili zina uhusiano, na wachambuzi wengi wa mambo wanaelewa kuwa, Israel inataka zaidi kuwepo na kudumisha uhusiano huo. Katika miaka ya hivi karibuni pia Israel na Saudia zimepeana ripoti nyingi za kipelelezi baada ya kuanza vita vya Syria hususan baada ya kuimarika ushawishi wa Iran katika nchi za Iraq na Syria."
Uhusiano wa pande hizo mbili umeenda mbali zaidi hadi Jenerali Gadi Eizenkot ambaye ni Mkuu wa Majeshi ya Israel kutangaza waziwazi kuwa, utawala huo daima uko tayari kutoa ushauri na msaada kwa Saudi Arabia kwa ajili ya kukabiliana na Iran na ushawishi wa nchi hiyo katika eneo la Mashariki ya Kati. Suala hilo pia limekaririwa mara kadhaa na Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu.
Katika miezi ya hivi karibuni kumeshuhudiwa harakati za kukaribiana zaidi tawala hizo mbili za Riyadh na Tel Aviv na kushiriki katika vikao na midahalo ya moja kwa moja, jambo ambalo halikuwa likifanyika waziwazi katika miaka ya nyuma. Hata hivyo inaonekana kuwa, kuwepo adui wa pamoja wa pande hizo mbili yaani Iran, kumerahisisha sana jambo hilo.
Kwa sasa pia timu ya serikali ya Saudi Arabia inayoongozwa na Muhammad bin Salman, mrithi wa kiti kijana, mwanagenzi na anayeandamwa na kashfa nyingi, imetoa pendekezo la kuimarishwa zaidi uhusiano na utawala unaoua Waislamu na watoto wa Palestina wa Israel, suala ambalo kwa njia moja au nyingine limechangia katika uamuzi uliochukuliwa na Rais Donald Trump wa Marekani wa kutangaza Quds tukufu kuwa mji mkuu wa Israel. Suala hili limewachukiza sana walimwengu hususan wachambuzi wa mambo kiasi kwamba, gazeti la Raiyul Youm linalochapishwa mjini London kwa lugha ya Kiarabu limechalisha Makala iliyoandikwa na mhariri wake mkuu, Abdul Bari Atwan akisema: Sasa kutamka jina la Jumuiya ya Nchi za Kiarabu kunatia kichefuchefu.