Padri raia wa Marekani apandishwa kizimbani Uturuki kwa tuhuma za ugaidi
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i43182-padri_raia_wa_marekani_apandishwa_kizimbani_uturuki_kwa_tuhuma_za_ugaidi
Padri mmoja raia wa Marekani amepandishwa kizimbani nchini Uturuki kwa kujihusisha na harakati za kigaidi ndani ya taifa hilo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Apr 16, 2018 09:49 UTC
  • Padri raia wa Marekani apandishwa kizimbani Uturuki kwa tuhuma za ugaidi

Padri mmoja raia wa Marekani amepandishwa kizimbani nchini Uturuki kwa kujihusisha na harakati za kigaidi ndani ya taifa hilo.

Kesi ya padri huyo aliyejulikana kwa jina la Andrew Brunson, imeanza kusikilizwa katika mji wa İzmir magharibi mwa Uturuki ambako kuna kanisa analoliongoza. Brunson alitiwa mbaroni na maafisa usalama wa Uturuki mwezi Oktoba 2016 akiwa pamoja na mke wake.

Taarifa iliyotolewa na serikali ya Uturuki inasema kuwa, padri huyo alikuwa akiifanyia kazi harakati ya Fethullah Gülen, mtuhumiwa nambari moja wa jaribio la mapinduzi yaliyofeli ya mwezi Julai mwaka 2016 nchini humo. Vilevile ametuhumiwa kuwa anashirikiana na chama cha Kikurdi cha PKK ambacho serikali ya Ankara inasema ni kundi la kigaidi. Andrew Brunson ametuhumiwa kufanya ujasusi dhidi ya serikali ya Uturuki. 

Trump alipokutana na Rais Recep Tayyip Erdoğan bila kufikia mwafaka

Kutiwa mbaroni padri huyo raia wa Marekani ni jambo jingine lililochafua uhusiano wa Ankara na Washington suala ambalo pia lilijadiliwa na marais wa nchi hizo mbili wakati walipokutana na wakashindwa kufikia mwafaka.

Mwezi Septemba mwaka jana Rais Recep Tayyip Erdoğan wa Uturuki alitangaza kwamba, iwapo Marekani itakubali kuikabidhi serikali yake Fethullah Gülen, nayo itamwachilia huru Andrew Brunson, suala ambalo lilipingwa na Washington.