Baraza la Usalama latakiwa kuichukulia hatua Israel kwa kuwaua Wapalestina
Balozi wa Palestina katika Umoja wa Mataifa amelitaka Baraza la Usalama la umoja huo liuchukulie hatua mara moja utawala wa Kizayuni wa Israel kwa kuendelea kuwaua shahidi Wapalestina wanaofanya maandamano ya amani katika mpaka wa Ghaza.
Riyad Mansour alitoa mwito huo jana Ijumaa mjini New York, saa chache baada ya wanajeshi wa Kizayuni kuwaua shahidi Wapalestina wengine watatu na kuwajeruhi wengine zaidi ya 800, kwa kushiriki maandamano ya amani katika mpaka wa Gaza.
Amesema, "Tuna haki ya kuandamana kwa amani, maandamano ya wiki hii yamekuwa makubwa kuliko ya wiki jana, na yanazidi kuimarika kila uchao, kwa kuwa Wapalestina ni watu wastaarabu na wenye kudhihirisha maoni yao kishujaa, na katu hawastahili risasi za Wazayuni."
Kadhalika mjumbe huyo wa Palestina katika UN amesisitiza kuwa, lazima watenda jinai wote wa Israel wakabiliwe na mkono wa sheria kutokana na ukatili walioufanya dhidi ya Wapalestina, huku akiishangaa jamii ya kimataifa kwa kuendelea kufumbia macho jinai hizo za kutisha.
Ukatili wa jana Ijumaa wa jeshi la utawala haramu wa Israel dhidi ya waandamanaji wa Kipalestina umefanyika muda mfupi baada ya Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa kuijia juu Tel Aviv kwa kutumia nguvu kupita kiasi kukabiliana na waandamanaji hao wa Kipalestina, huku Amnesty International ikitoa mwito wa kuwekewa vikwazo vya silaha utawala huo khabithi.
Idadi ya Wapalestina waliouawa shahidi kwa kushiriki maandamano ya amani ya 'Haki ya Kurejea' tokeo Machi 30 hadi sasa imepindukia 38.