Syria: Riyadh ingali inawazuia raia wetu kwenda kufanya Hija
Serikali ya Syria imeukosoa vikali utawala wa Aal-Saud kwa kuingiza siasa katika amali tukufu ya Hija, ambapo Riyadh imewazuia raia wa Syria kwenda kutekeleza ibada hiyo kwa mwaka wa saba mfululizo.
Wizara ya Waqfu ya Syria imesema katika taarifa kwamba, Saudi Arabia ingali inawawekea vizingiti na masharti mazito raia wa Syria wanaotaka kwenda katika nchi hiyo kuhiji.
Saudia na Syria hazijakuwa na uhusiano wa kidiplomasia tokeo mwaka 2012.
Mapema mwezi huu, serikali ya Saudi Arabia iliendelea kuitumia ibada hiyo ya Hija kisiasa kwa kuweka masharti kadhaa yaliyowazuia Waislamu kutoka Qatar kwenda kutekeleza Umra katika mwezi uliopita wa Ramadhani.
Moja ya masharti hayo ni kuwalazimisha raia wa nchi hiyo waliotaka kwenda kufanya Umra mwaka huu kusafiri kutokea nje ya Qatar na kuingia nchini Saudi Arabia kwa njia ya anga kupitia uwanja wa ndege wa Mfalme Khalid.
Hii ni katika hali ambayo miezi kadhaa iliyopita Saudia iliwarejesha kwa kutumia uwanja wa ndege wa Khalid bin Abdulaziz, raia wa Qatar waliokuwa wameingia katika ardhi ya nchi hiyo kwa ajili ya kutekeleza ibada ya Umra kutokea Kuweit.
Siku chache zilizopita, Jumuiya ya Maimamu wa Swala za Jamaa nchini Tunisia ilitoa taarifa ikisisitiza kuwa Saudi Arabia inatumia mapato yanayotokana na ibada ya Hija kwa ajili ya kuzishambulia nchi nyingine za Kiislamu.