Ndege za kivita za Saudia zaua raia 5 nchini Yemen
Kwa akali raia watano Wayemen wameuawa kufuatia mashambulio mapya ya ndege za kivita za utawala wa Saudia katika mkoa wa Tai'zz wa kusini magharibi mwa Yemen.
Kwa mujibu wa Televisheni ya al-Masirah, Jumamosi ya leo ndege za kivita za Saudia zimedondosha mabomu katika wilaya ya Dhubab yapata kilomita 350 kusini mwa mji mkuu Sana'a na kuua watu watano.
Ripoti hiyo imeongeza kuwa, wanawake watatu na mtoto mmoja ni kati ya raia hao waliouawa.
Aidha jana Ijumaa, ndege za kivita za Saudia zilishambulia wilaya ya al-Ghil katika mkoa wa Jawf kaskazini mwa Yemen.
Hadi sasa watu wasiopungua 9,400 wameshauawa na wengine zaidi ya 16,000 wamejeruhiwa tangu Saudia na washirika wake walipoanzisha mashambulio na uvamizi wa kijeshi dhidi ya Yemen mwezi Machi mwaka jana kwa lengo la eti kumrejesha madarakani kibaraka wa utawala wa Aal Saud, Rais wa nchi hiyo aliyejiuzulu na kuitoroka nchi Abd Rabbuh Mansur Hadi. Mashambulio hayo yameangamiza na kusababisha hasara kubwa kwa miundombinu ya Yemen, mbali na kulenga na kubomoa hospitali, shule, misikiti na turathi za kihistoria za nchi hiyo.