Jeshi la Israel lawapiga risasi makumi ya wanafunzi wa Kipalestina
Makumi ya wanafunzi wa Palestina wanauguza majeraha baada ya kumiminiwa risasi na wanajeshi katili wa utawala wa Kizayuni katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan.
Duru za habari zinasema kuwa, askari wa utawala haramu wa Israel jana Jumapili waliivamia Shule ya Sekondari ya Tuqu, yapata kilomita 12 kusini mashariki mwa Baitu Lahm, katikati ya Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na kujeruhi makumi ya wanafunzi kwa kuwapiga risasi.
Habari zaidi zinasema kuwa, wanajeshi hao wa utawala haramu wa Israel waliwakamata na kuwazuilia kwa muda walimu na wafanyakazi wa shule hiyo, akiwemo mwalimu mkuu.
Wapalestina haswa wa Ukanda wa Ghaza tangu tarehe 30 Machi mwaka huu hadi sasa wamekuwa wakifanya maandamano ya amani ya Haki ya Kurejea kwa lengo la kuhitimisha ukaliaji mabavu wa utawala huo ghasibu na kuvunja mzingiro katika eneo hilo.

Kadhalika wamekuwa wakiandamana kulalamikia hatua ya Marekani ya kuuhamishia ubalozi wake katika mji mtukufu wa Quds kutoka Tel Aviv, kitendo ambacho kilikabiliwa na maandamano katika kila kona ya Palestina na katika nchi za Kiislamu kama vile Iran, Uturuki, Misri, Jordan, Tunisia, Algeria, Iraq na Morocco.
Kadhalika Disemba 21 mwaka jana, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilipigia kura kwa kishindo, azimio la kulaani kitendo hicho cha Marekani na kuitaja kama sera tatanishi.