Lieberman: Hakuna anayeweza kuiangamiza Hamas kwa nguvu
Waziri wa Vita wa utawala wa Kizayuni aliyejiuzulu amesema kuwa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina Hamas haiwezi kusambaratishwa huko Ghaza kwa kutumia nguvu za kijeshi.
Akizungumza katika mahojiano na kanali ya 12 ya televisheni ya utawala wa Kizayuni, Lieberman amesema kuwa Israel imekuwa ikitafuta mbinu na njia mbadala za kuiangamiza harakati ya Hamas kwa kuwa ilikuwa haiwezi kuipindua harakati hiyo kwa kutegemea vita.
Lieberman ameashiria namna siasa zake dhidi ya Ghaza zilivyokuwa zikikabiliwa na ukosoaji wa viongozi wengine wa Israel na kueleza kuwa Israel ilijaribu kwanza kupunguza makali ya mzingiro katika Ukanda wa Ghaza na kisha kujongea katika mazungumzo ya moja kwa moja na wakazi wa eneo hilo na hivyo kuweza kuifuta Hamas katika mlingano huo.
Avigdor Lieberman Jumatano iliyopita baada ya Israel kukubali usitishaji vita kufuatia mashambulizi ya makombora ya makundi ya muqawama ya Palestina alitangaza kuwa, usitishaji vita huo una maana ya kusalimu amri na akatangaza kujiuzulu nafasi yake ya Waziri wa Vita wa utawala wa Kizayuni. Siku kadhaa zilizopita wanamuqawama wa Palestina walivurumisha karibu makombora 500 na roketi kuelekea katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu ikiwa ni radiamali yao kwa mashambulizi ya Wazayuni huko Ukanda wa Ghaza.