Nov 28, 2018 07:39 UTC
  • Indhari ya Unicef kuhusu hali mbaya ya watoto wa Afghanistan

Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa Unicef umeonya kuhusu kuendelea kuwa mbaya hali ya watoto wa Afghanistan, ambao wanakodolewa macho na ghasia na umwagaji damu kila uchao.

Alison Parker, Mkuu wa Mawasiliano wa Unicef nchini Afghanistan amesema kuwa, hii leo watu milioni sita nchini Afghanistan wanahitaji msaada wa dharura, na kwamba asilimia 50 kati yao (milioni 3) ni watoto wadogo.

Amesema watoto 5,000 wa Kiafghani wameuawa au kujeruhiwa katika robo tatu ya kwanza ya mwaka huu 2018, huku akikumbusha kuwa, ghasia hizo nchini Afghanistan zitatimiza mwaka 40 mwaka ujao 2019. 

Afisa huyo wa Unicef amesema machafuko, ghasia, umwagaji damu na hali mbaya ya binadamu zimewafanya watoto milioni tatu nchini humo kutokuwepo shuleni, ambapo aslimia 60 ya idadi hiyo ni wasichana.

Askari vamizi wa Marekani katika mashamba ya mihadarati nchini Afghanistan

Mwishoni mwa mwezi uliopita, wananchi wa Afghanistan katika mkoa wa Nangarhar, mashariki mwa nchi hiyo walifanya maandamano dhidi ya askari wa kigeni, wanaoongozwa na Marekani, wakisisitiza kuwa, uwepo wa askari hao wa kigeni ndio chanzo cha ukosefu wa usalama na amani, ongezeko la makundi ya kigaidi na kadhalika ongezeko la uzalishaji wa madawa ya kulevya katika nchi hiyo.

Mwaka 2001, Marekani ilituma wanajeshi wake kwenda kuivamia Afghanistan kwa madai ya kupambana na ugaidi, kuleta amani ya kudumu na kuwaandalia mazingira na maisha bora wananchi wa Afghanistan.

Tags