Dec 08, 2018 07:57 UTC
  • Serikali mpya ya Bahrain; dhihirisho la nembo kubwa zaidi ya Udikteta

Baada ya kufanyika uchaguzi wa kimaonyesho wa bunge nchini Bahrain, Mfalme Hamad bin Isa Aal Khalifa amemkabidhi tena jukumu la kuunda serikali mpya, mtu yule yule ambaye anajulikana kuwa waziri mkuu pekee katika historia ya nchi hiyo.

 Khalifa bin Salman Aal Khalifa

Uchaguzi wa bunge la sita la Bahrain ulifanyika katika awamu mbili za tarehe 24 Novemba na tarehe Mosi Desemba mwaka huu, ambapo ni wananchi wachache mno waliojitokeza kupiga kura.

Tangu ilipopata uhuru wake mwaka 1971 hadi sasa, Bahrain imeshafanya jumla ya chaguzi sita za bunge.

Uchaguzi wa kwanza wa bunge nchini Bahrain ulifanyika mwaka 1973 na chaguzi nyingine za bunge la nchi hiyo zilifanyika mwaka 2002, 2006, 2010, 2014 na mwaka huu wa 2018.

Uchaguzi wa mwaka huu haukukidhi hata kipimo kimoja cha uchaguzi huru, zaidi ya kuwa "onyesho la uchaguzi" tu lililoigizwa na aila ya Aal Khalifa; kwa sababu vuguvugu kubwa zaidi la upinzani nchini humo, yaani Harakati ya Kiislamu na Kitaifa ya Al-Wifaq ilivunjwa mwaka 2016 na utawala huo wa kiimla, viongozi wake wa kisiasa na kidini ama wakanyang'anywa uraia au wakahukumiwa vifungo vya miaka mingi jela, sambamba na kunyimwa haki zao za msingi za kiraia.

Zoezi la upigaji kura katika uchaguzi wa bunge la Bahrain

Kwa sababu hiyo, makundi na wananchi wengi wa Bahrain, ambao walikuwa wanalijua lengo la igizo hilo la kisiasa la utawala wa Aal Khalifa waliususia uchaguzi wa bunge wa mwaka huu. Kwa kuitisha uchaguzi wa bunge, utawala wa Aal Khalifa ulitaka kuonyesha kuwa ungali una uhalali kisheria wa kuitawala Bahrain; na ndiyo maana umedai eti asilimia 70 ya wananchi waliotimiza masharti, walijitokeza kupiga kura, ilhali idadi halisi ya waliopiga kura ilikuwa chini ya asilimia 30.

Wapinzani wameuita uchaguzi huo wa bunge "mbwembwe za kidemokrasia za nembo ya udikteta wa eneo". Nayo kanali ya televisheni ya DW ya Ujerumani, imeuelezea uchaguzi wa Bahrain kama "jitihada za kuelekea kwenye demokrasia ndani ya anga ya ukandamizaji." 

Mfalme Hamad bin Isa Aal Khalifa

Ukweli ni kwamba demokrasia imekejeliwa na kufanywa kitu cha dhihaka na mfalme wa Bahrain Hamad bin Isa Aal Khalifa, kiasi cha kufika hadi ya kutokuwa tayari kumwondoa kwenye wadhifa wa uwaziri mkuu, ami yake mwenye umri wa miaka 83, aliyeshikilia kiti hicho kwa muda wa miaka 47, kwa kumkabidhi tena jukumu la kuongoza serikali mpya ya nchi hiyo.

Waziri Mkuu wa Bahrain, Khalifa bin Salman Aal Khalifa, amekuwa akishikilia nafasi ya juu ya madaraka kwa muda mrefu zaidi kuliko shakhsia yeyote wa kisiasa duniani, kiasi kwamba anaweza kutajwa kama "nembo kuu ya udikteta".

Nukta nyingine ni kwamba, kati ya mawaziri wote 18 wa serikali yake, Khalifa bin Salman amewabadilisha mawaziri watatu tu, ili kuzidi kuthibitisha kuwa, kufanyika uchaguzi hata wa kimaonyesho nchini Bahrain hakuna taathira yoyote katika uteuzi wa baraza la mawaziri la nchi hiyo.

Kuhusiana na suala hilo, Muhammad Ali Al-Houthi, Mkuu wa Kamati Kuu ya Mapinduzi ya Yemen ameashiria katika ukurasa wake wa Twitter hatua iliyochukuliwa na mfalme wa Bahrain ya kumpa ami yake  Khalifa bin Salman Aal Khalifa jukumu la kuunda serikali kwa kuandika: "Kwa mara ya 11 Mfalme wa Bahrain amemkabidhi aliyekuwa waziri mkuu wa nchi hiyo Khalifa bin Salman Aal Khalifa jukumu la kuunda serikali. Tunaweza kusema, kwa uchache, matunda ya kuitisha uchaguzi wa kiagizo na kimaonyesho nchini humo yangeweza kuwa ni kuteuliwa waziri mkuu mpya."

Salman bin Hamad bin Isa Aal Khalifa, mrithi wa ufalme wa Bahrain

Suala jengine ni kwamba, kwa amri ya mfalme, mrithi wa kiti hicho Salman bin Hamad bin Isa Aal Khalifa, ameteuliwa kuwa Naibu Waziri Mkuu.

Maana ya uteuzi huo ni kwamba, endapo Khalifa bin Salman atashindwa kuendelea kushika wadhifa wa uwaziri mkuu kwa sababu yoyote ile, iwe ya uzee au kifo, hatamu za uongozi wa serikali zitaingia mikononi mwa mwana wa kiume wa mfalme wa Bahrain; na kwa utaratibu huo, madaraka ya nchi yatarasimishwa kikamilifu ndani ya aila ya Sheikh Hamad bin Isa Aal Khalifa.../

Tags