Daesh yafanya mauaji mengine ya kimbari, yaua wafungwa 700
Kundi la kigaidi la Daesh limefanya mauaji mengine ya kutisha huko mashariki mwa Syria kwa kuua wafungwa mia saba karibu na eneo lililoko kwenye mpaka wa nchi hiyo na Iraq.
Taasisi ya haki za binadamu nchini Syria imeripoti kuwa, kundi hilo la Daesh limeua wafungwa wapatao mia saba katika kipindi cha miezi mwili karibu na mpaka wa nchi hiyo na Iraq.
Taasisi hiyo yenye makao yake makuu London huko Uingereza imesema wafungwa hao 700 walikuwa sehemu ya raia na wapiganaji 1350 waliokuwa wakishikiliwa na kundi la kigaidi la Daesh kandokandio ya mji wa Hajin.
Kundi la Daesh linadhibiti eneo dogo la ardhi ya mashariki mwa mto Furati (Euphrates) nchini Syria ambalo limevamiwa na wapiganaji wa kundi la SDF linalosaidiwa na Marekani.
Eneo hilo limekuwa likishuhudia mapigano makali kwa miezi miwili sasa baina ya makundi hayo mawili.
Kiongozi wa kundi hilo la SDF amewaambia waandishi habari kwamba, wapiganaji wasiopungua elfu tano wa kundi la kigaidi la Daesh bado wapo katika eneo hilo na kwamba wengi wao ni raia wa kigeni ambao wako tayari kupigana hadi kufa.