Hamas yalaani azma ya Abbas ya kulivunja Bunge la Palestina
Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina (Hamas) imekosoa vikali mpango wa Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina, Mahoud Abbas wa kulivunja Bunge, ikisisitiza kuwa kitendo hicho hakitakuwa na matokeo mengine ghairi ya kushadidisha migawanyiko miongoni mwa makundi ya Palestina.
Yehya Musa, kiongozi wa ngazi za juu wa Hamas ambaye pia mwanachama wa Baraza la Bunge la Palestina amesema azma hiyo ya Abbas mbali na kuzusha hitilafu kati ya makundi ya Kipalestina, lakini pia itavuruga mfumo wa kisiasa wa Palestina.
Kauli hiyo ya Hamas imetolewa masaa machache baada ya Mahmoud Abbas kutangaza kuwa, serikali yake inapania kutekeleza uamuzi wa Mahakama ya Katiba wa kulivunja Bunge la Palestina na kuitisha uchaguzi wa Bunge katika kipindi cha miezi sita ijayo.
Ifahamike kuwa, Baraza la Kutunga Sheria la Palestina (Bunge) lina wanachama wengi wa Hamas, ambao wanaliongoza tangu harakati hiyo ishinde uchaguzi mkuu wa mwaka 2006.
Wiki iliyopita, Hamas ilisisitiza kuwa, kushiriki kwa wingi mamia ya maelfu ya watu katika maadhimisho ya mwaka wa 31 tangu kuasisiwa harakati hiyo ni ishara mpya ya uungaji mkono wa wananchi wa Palestina kwa mapambano ya ukombozi dhidi ya Wazayuni maghasibu.