Mpalestina afa shahidi gerezani Israel baada ya kunyimwa matibabu
Mfungwa Mpalestina amekufa shahidi akiwa katika gereza la utawala wa Kizayuni wa Israel baada ya kunyimwa matibabu.
Fares Baroud, aliyekuwa mkaazi wa kambi ya wakimbizi ya al-Shati kaskazini mwa Ukanda wa Ghaza alipoteza maisha mapema Jumatano kutokana na hatua ya wakuu wa magereza kumnyima idhini ya kupata matibabu ya dharura. Maplestina huyo aliyekuwa na umri wa miaka 51 alikuwa na matatizo ya ini lakini wakuu wa gereza walikataa kumpa matibabu ya haraka.
Mkurugenzi wa Idara ya Habari ya Wafungwa Wapalestina, Nahed al-Fakhouri amesema kifo cha Baroud mikononi mwa maafisa wa utawala haramu wa Israel ni jinai kubwa na inaashiria sera za kihalifu zinazotekelezwa na Idara ya Magereza ya Israel dhidi ya wafungwa Wapalestina.
Nayo Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina, Hamas, imesema utawala wa Kizayuni wa Israel unabeba dhima ya kifo cha mfungwa huyo. Hamas imesema wakuu wa magereza ya Israel wanawatelekeza wafungwa Wapalestina jambo ambalo ni jinai dhidi ya binadamu. Hamas imetoa wito kwa jumuiya za kimataifa kuchukua hatua za dharura ili kuokoa maisha ya maelfu ya wafungwa Wapalestina wanaoshikiliwa katika magereza za kuogofya ya Israel. Aidha Hamas imesema jinai hizo za Israel haziwezi kuvunja irada ya Wapalestina wanaopigania ukombozi wa ardhi zao.