Wapalestina wazitaka nchi za Kiarabu zisusie mkutano wa Poland
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i51510-wapalestina_wazitaka_nchi_za_kiarabu_zisusie_mkutano_wa_poland
Waziri wa Mambo ya Nje wa Palestina ametoa mwito kwa nchi za Kiarabu kususia mkutano wa Poland, ulioitishwa na kufadhiliwa na Marekani.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 12, 2019 10:47 UTC
  • Wapalestina wazitaka nchi za Kiarabu zisusie mkutano wa Poland

Waziri wa Mambo ya Nje wa Palestina ametoa mwito kwa nchi za Kiarabu kususia mkutano wa Poland, ulioitishwa na kufadhiliwa na Marekani.

Riadh al-Maliki amenukuliwa na shirika la habari la AP akisema kuwa, iwapo Waarabu lazima washiriki mkutano huo, kwa uchache wanapaswa kutuma maafisa wa ngazi za chini.

Saudi Arabia na Umoja wa Falme za Kiarabu ni miongoni mwa nchi za Kiarabu zitakazotuma mawaziri wao wa mambo ya nje katika mkutano huo ambao utahudhuriwa pia na Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Palestina amebainisha kuwa, Wapelestina wanautazama mkutano huo wa Februari 13 na 14 kama njama dhidi ya kadhia ya Palestina, na hivyo wangelipenda kuona nchi za Kiarabu zikiususia.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Mike Pompeo na Netanyahu watashiriki mkutano huo

Siku chache zilizopita, Saeb Erakat, Katibu wa Kamati ya Utendaji ya Harakati ya Ukombozi wa Palestina (PLO) aliandika kwenye ukurasa wake wa Twitter kuwa, "Msimamo wetu uko wazi, hatutashiriki kongamano hilo, na wala hatujamtuma mtu yeyote kwenda kuzungumza kwa niaba ya Palestina."

Wizara ya Mambo ya Nje ya Palestina kwa upande wake imeutaja mkutano huo wa Warsaw kama njama za Marekani za kutaka kuwashawishi watakaoshiriki kuidhinisha sera na mitazamo ya Washington kuhusu eneo la Mashariki ya Kati, haswa kadhia ya Palestina.