Israel kumpa chakula kwa nguvu mfungwa wa Kipalestina
Utawala haramu wa Kizayuni umepasisha mpango wa kumpa chakula kwa nguvu mwandishi wa habari raia wa Palestina ambaye anashikiliwa katika jela za utawala huo.
Shirika la habari la Farsi limeripoti kuwa Issa Qaraqeh Mkuu wa kitengo cha kushughulikia wafungwa na raia wa Palestina walioachiwa huru amesema kuwa utawala wa Kizayuni umeamua kumpa chakula kwa nguvu mwandishi habari wa Kipalestina kwa jina la Muhammad al Qiq ambaye amefungwa katika jela za utawala huo. Muhammad al Qiq amekuwa akigoma kula chakula kwa siku ya 71 sasa. Israel imechukua uamuzi huo huku kitendo cha kumlazimisha kwa nguvu mtu kula chakula kikitambuliwa kuwa kinyume na sheria za kimataifa na aina ya utesaji wa kimwili.
Muammad al Qiq leo Jumatao amepoteza kabisa uwezo wa kuzungumza huku jicho lake moja likiwa halioni. Mwandishi huyo wa habari wa Kipalestina aliwahi kutamka kuwa ni lazima aachiwe huru na utawala wa Kizayuni au afe shahidi katika njia hiyo. Mwezi Novemba mwaka jana vikosi vya utawala wa Kizayuni wa Israel vilimtia mbaroni Mohammad al Qiq aliye na umri wa miaka 33 akiwa nyumbani kwake Ramallah katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan.