Rais wa Iraq: Hatutairuhusu Marekani itumie ardhi yetu kuishambulia Iran
Rais Barham Salih wa Iraq amesema katu nchi hiyo ya Kiarabu haitairuhusu Marekani itumie ardhi yake kuanzisha shambulizi lolote la kijeshi dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Rais wa Iraq alisema hayo jana Jumanne katika mahojiano na televisheni ya CNN mjini London na kuongeza kuwa, kamwe Iraq haitokubali kubadilishwa na kuwa sehemu ya kupangia njama za kuwachokoza majirani zake na amesisitiza kwamba urafiki wa Iran na Iraq umejengeka juu ya misingi ya kuheshimiana na kulinda manufaa ya pande mbili.
Amesema vikosi vya Marekani vipo nchini Iraq kwa lengo moja tu, nalo ni kupambana na magaidi wa kundi la ukufurishaji la Daesh (ISIS). Rais wa Iraq amesema hayo alipoulizwa kuhusu kauli ya Rais Donald Trump aliyedai mwezi Februari mwaka huu kuwa jeshi la nchi hiyo liko Iraq kwa ajili ya kufuatilia nyendo na harakati za Iran.
Rais wa Iraq ameeleza bayana kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni jirani mwema na muhimu ambaye ilisaidia sana kuutokomeza utawala wa kidikteta wa Saddam Hussein na pia katika kuliangamiza kundi la kigaidi na ukufurishaji la Daesh (ISIS) nchini mwake.
Kuhusu mgogoro na taharuki ya hivi sasa kati ya Iran na Marekani, Rais wa Iraq ameonya kuwa, "Ni rahisi kuanzisha vita, lakini ni vigumu sana kuvihitimisha."
Baada ya Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu kutungua drone ya kijasusi ya Marekani iliyoingia katika anga yake hivi karibuni, Trump alidai kuwa alisitisha shambulizi la ulipizaji kisiasa wa hatua hiyo ya Iran dakika chache kabla ya kutekelezwa, na kisha baadaye akadai kuwa shambulizi hilo halijafutwa bali limeakhirishwa tu.