Hamas: Waziri wa Mambo ya Nje wa Bahrain ameisaliti Palestina
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i54878-hamas_waziri_wa_mambo_ya_nje_wa_bahrain_ameisaliti_palestina
Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina HAMAS imekosoa vikali kitendo cha Waziri wa Mambo ya Nje wa Bahrain, Khalid bin Ahmad bin Muhammad Aal Khalifa cha kukukata na kufanya mazungumzo hadharani na mwenzake wa utawala haramu wa Israel, Israel Katz nchini Marekani.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 20, 2019 03:17 UTC
  • Hamas: Waziri wa Mambo ya Nje wa Bahrain ameisaliti Palestina

Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina HAMAS imekosoa vikali kitendo cha Waziri wa Mambo ya Nje wa Bahrain, Khalid bin Ahmad bin Muhammad Aal Khalifa cha kukukata na kufanya mazungumzo hadharani na mwenzake wa utawala haramu wa Israel, Israel Katz nchini Marekani.

Msemaji wa HAMAS, Sami Abu Zuhri ameitaja hatua hiyo kama usaliti wa wazi kwa Wapalestina na matukufu ya Kiislamu. Katika ujumbe wake kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter, afisa huyo wa ngazi za juu wa HAMAS ameandika kuwa, "Mikutano ya aina hiyo ni sawa na kusaliti Palestina na mji mtukufu wa Quds. Mikutano hii kamwe haiwezi kupotosha ufahamu wa taifa hilo na kulisukuma liachane na kadhia ya Palestina na likumbatie suala la kufanywa wa kawaida uhusiano na utawala wa Kizayuni."

Wakati huohuo, harakati ya Kiislamu ya al-Wefaq nchini Bahrain pia imekosoa mkutano huo wa Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo na mwenzake na utawala ghasibu wa Israel mjini Washington Julai 17 na kuelekeza bayana kuwa, kikao hicho ni fedheha na dhambi isiyosameheka.

Katika mkutano huo, waziri huyo wa Bahrain alikariri tena madai yake kwamba kuanzishwa uhusiano wa nchi hiyo na utawala haramu wa Israel ndio 'msingi wa amani halisi' katika eneo la Asia Magharibi.

Bahrain kama tawala zingine vibaraka za Kiarabu imekuwa ikifanya jitihada za kuwa na uhusiano wa kawaida na Israel

Mwezi uliopita, Waziri wa Mambo ya Nje wa Bahrain alisema katika mahojiano na gazeti la The Times of Israel pambizoni mwa mkutano wa eti kuimarisha uchumi wa Wapalestina uliofanyika Manama kwamba, Bahrain inataka kuwa na amani na kuimarisha uhusiano wake na utawala huo haramu.

Sheikh Khalid bin Ahmed Al Khalifah alidai kuwa, "Israel ina haki kuwepo na itaendelea kuwepo bila shaka. Israel ni sehemu ya turathi za eneo hili."