Jul 21, 2019 04:21 UTC
  • HAMAS yasisitiza kukomeshwa mashambulio ya Wazayuni dhidi ya Wapalestina

Msemaji wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS ametangaza kuwa, adui mzayuni ndiye anayebeba dhima ya kuendelea hujuma na mashambulio dhidi ya Wapalestina yakiwemo mashambulio dhidi ya waandamano wa maandamno ya "Haki ya Kurejea".

Fawzi Barhoum, msemaji wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS amesema kuwa, mashambulio ya risasi ya makusudi ya jeshi la utawala haramu wa Israel dhidi ya Wapalestina wanaoshiriki katika maandamano ya "Haki ya Kurejea" ambapo akthari ya wanaojeruhiwa ni wanawake na watoto ni jinai nyingine katika faili jeusi la Israel dhidi ya taifa la Palestina.

Kiongozi huyo mwandamizi wa wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS ametaka zichukuliwe hatua za kistratijia ili kuufanya utawala huo ghasibu ukomeshe jinai zake katika ardhi za Palestina unazozikalia kwa mabavu.

Aidha amesema kuwa, kumwagwa damu za Wapalestina ni mstari mwekundu na kwamba, wananchi wa Palestina katu hawatanyamazia kimya jinai za utawala dhalimu wa Israel.

Maandamano ya Wapalestina ya "Haki ya Kurejea"

Hivi karibuni, Shirika la Afya Duniani (WHO) lilitangaza kuwa, jumla ya Wapalestina 313 wameuawa na wanajeshi wa utawala wa Israel huko katika Ukanda wa Gaza Palestina tangu yalipoanza maandamano ya 'Haki ya Kurejea'.

Maandamano ya "Haki ya Kurejea" ya kupigania Wapalestina kurejea katika ardhi za mababu zao yalianza tarehe 30 Machi 2018 siku ambayo ilisadifiana na kumbukumbu ya "Siku ya Ardhi" huko Palestina. Maandamano hayo hufanyika kila Ijumaa katika mpaka wa Ukanda wa Gaza na maeneo mengine ya Palestina yanayokaliwa kwa mabavu na Wazayuni.

Tags