Hizbullah: Lebanon hatuna hofu na vitisho vya utawala haramu wa Israel
Naibu Katibu Mkuu wa Harakati ya Muqawama ya Hizbullah nchini Lebanon amesema kuwa, kwa kutegemea uwezo wake wa ndani, Lebanon haina hofu yoyote na vitisho vya utawala haramu wa Kizayuni.
Sambamba na kubainisha kwamba Lebanon imebadili sera yake ya kulalamika na kushtaki na kuwa sera ya muqawama na kujihami, Sheikh Naim Qassem ameongeza kwamba vitisho vya adui Mzayuni havijawa na taathira yeyote kwenye azma ya muqawama dhidi ya siasa za uvamizi za Israel.
Naibu Katibu Mkuu wa Harakati ya Hizbullah nchini Lebanon pia ameashiria nafasi ya Lebanon katika kivuli cha mlingano wa pande tatu za jeshi, taifa na muqawama kwa ajili ya kuunga mkono kujitawala na umoja wa ardhi yote ya nchi hiyo na kuongeza kwamba, muqawama umejiweka mbali na siasa na kwamba lengo lake kwa sasa ni kuzikomboa ardhi zinazokaliwa kwa mabavu na utawala ghasibu wa Israel.