Israel yakiri, Hizbullah imetungua ndege yake isiyo na rubani
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i55898-israel_yakiri_hizbullah_imetungua_ndege_yake_isiyo_na_rubani
Duru zenye mfungamano na utawala wa Kizayuni wa Israel zimethibitisha kuwa, wapiganaji wa Hizbullah ya Lebanon wametungua ndege isiyo na rubani ya utawala huo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Sep 09, 2019 06:56 UTC
  • Israel yakiri, Hizbullah imetungua ndege yake isiyo na rubani

Duru zenye mfungamano na utawala wa Kizayuni wa Israel zimethibitisha kuwa, wapiganaji wa Hizbullah ya Lebanon wametungua ndege isiyo na rubani ya utawala huo.

Vyombo vya habari vya utawala wa Kizayuni wa Israel vimenukuu duru za jeshi la utawala huo vikikiri kwamba Hizbullah imetungua ndege isiyo na rubani ya utawala wa Tel Aviv.

Jeshi la Israel limedai kuwa, ndege hiyo iliyotungiliwa na Hizbullah ilikuwa katika kutekeleza majukumu yake ya kawaida na kwamba hakuna wasiwasi juu ya kupakuliwa taarifa za kijasusi kutoka kwenye ndege hiyo. 

Mapema leo harakati ya Hizbullah ya Lebanon ilitoa taarifa ikitangaza kuwa, imetungua ndege isiyo na rubani ya utawala wa Kizayuni wa Israel kwa kutumia silaha mwafaka wakati ilipokuwa ikivuka mpaka wa Lebanon na ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na Israel.

Ndege isiyo na rubani na Israel

Taarifa ya Hizbullah imesema kuwa, ndege hiyo isiyo na rubani ya Israel imetungiliwa na kuangushwa katika anga ya kitongoji cha Ramyeh huko kusini mwa Lebanon.

Kabla ya hapo Katibu Mkuu wa Hizbullah Sayyid Hassan Nasrullah alikuwa ametahadharisha kwamba, zama za ndege zisizo na rubani za Israel kuingia na kutamba katika anga ya Lebanon zimepita na kuyoyoma.