Aoun atetea oparesheni ya Hizbullah dhidi ya utawala wa Kizayuni
Rais wa Lebanon amekutana na Mjumbe wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya Lebanon na kutetea oparesheni iliyofanywa na harakati ya Hizbullah ya nchi hiyo dhidi ya chokochoko za utawala wa Kizayuni.
Rais Michel Aoun wa Lebanon amekutana na kufanya mazungumzo na Jan Kubis Mjumbe wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya Lebanon na kuashiria uchokozi wa mara kwa mara wa utawala wa Kizayuni huko Lebanon. Rais Aoun amekosoa kimya cha baadhi ya nchi mbele ya mashambulizi na chokochoko za Israel na radiamali zilizotolewa na nchi hiyo baada ya Hizbullah kuishambulia gari ya deraya ya utawala wa Kizayuni.
Rais Michel Aoun amesema kuwa Israel siku zote inatekeleza mashambulizi ya nchi kavu, anga na baharini dhidi ya Lebanon; ambapo mashambulizi ya karibuni kabisa ya utawala huo yalitekelezwa Agosti 25. Ndege mbili zisizo na rubani za Israel zilizokuwa na mabomu ya kuripuka zilishambulia eneo la kusini la Dahieh.
Rais wa Lebanon ameongeza kuwa nchi hiyo inafanya juhudi pakubwa kulinda azimio nambari 1701 la Baraza la Usalama hata hivyo itajibu uchokozi wowote dhidi yake kwa sababu inafahamu kuwa, ina haki ya kujilinda; na hiyo ni haki ambayo haiwezi kupuuzwa. Aoun amesisitiza kwa mara nyingine tena kwamba, Lebanon ina haki ya kurejeshewa ardhi zake zilizoghusubiwa huko Golan, mashamba ya Shaba'a, miinuko ya Kafr Shaba na kaskazini mwa mji wa Ghajar. Amesisitiza pia kuhusu kurejea nyumbani wakimbizi wa Syria.