Safari ya ghafla ya Waziri wa Ulinzi wa Marekani nchini Afghanistan
Akiwa katika kampeni zake za uchaguzi wa mwaka 2016, Rais Donald Trump wa Marekani aliahidi kuwa angewatoa askari wa nchi hiyo huko Afghanistan, lakini mwenendo huo umekumbwa na vizingiti vingi ambapo hadi sasa hajaweza kutekeleza ahadi hiyo.
Pamoja na hayo viongozi wa ngazi za juu wa serikali ya rais huyo wamekuwa wakifanya safari nchini Afghanistan na kufanya mazungumzo kuhusiana na suala hilo. Katika uwanja huo, Jumapili iliyopita Mark Esper, Waziri wa Ulinzi wa Marekani alifanya safari yake ya kwanza huko Kabul, mji mkuu wa nchi hiyo. Katika safari hiyo Esper aliwaeleza waandishi wa habari kwamba: "Lengo ni kuhakikisha mapatano ya amani yanafikiwa, mapatano ya kisiasa, ambayo ndio njia bora kuelekea mbele." Aidha Waziri huyo wa Ulinzi wa Marekani alidai kwamba Marekani inaweza kupunguza askari 8600 kati ya askari wa nchi yake walio Afghanistan, bila kuathiri mapambano dhidi ya ugaidi ndani ya nchi hiyo. Pamoja na hayo Mark Esper anaamini kwamba kuondoka askari hao kutatekelezeka tu iwapo kutafikiwa makubaliano na kundi la Taleban. Hii ni katika hali ambayo kundi la Taleban daima limekuwa likisisitizia kuondoka kikamilifu askari wa kigeni kutoka nchi hiyo. Hivi sasa Marekani ina jumla ya askari elfu 14 nchini Afghanistan. Wiki chache zilizopita Mark Esper alidai kwamba pamoja na kwamba nchi yake inafanya juhudi za kufikiwa makubaliano ya kisiasa na kundi la Taleban, lakini juhudi hizo hazina maana kwamba Washington itakuwa ikiamiliana na kundi hilo katika kila jambo.
Kuhusiana na suala hilo Esper alisema: "Tunataka tupate uhakika wa kufikiwa makubaliano yanayofaa." Mazungumzo ya amani nchini Afghanistan kati ya Marekani na kundi la Taleban ambayo yameendelea kwa karibu miezi tisa sasa, yalisimamshwa kwa upande mmoja na Trump hapo tarehe 7 Septemba mwaka huu, baada ya Taleban kutekeleza shambulio lililopelekea askari mmoja wa Kimarekani kuuawa. Kama makubaliano kati ya pande mbili yangefikiwa, basi kungewekwa wazi muda wa miezi 16 wa kuondoka askari wa Marekani kutoka Afghanistan. Serikali ya Trump kwa kuzingatia stratijia yake iliyofeli nchini Afghanistan na baada ya kukata tamaa ya kupatikana ushindi wa kijeshi ndani ya nchi hiyo, miaka kadhaa iliyopita iliingia katika mazungumzo ya moja kwa moja na kundi la Taleban huko Qatar kwa lengo la kulishirikisha kundi hilo la kigaidi katika serikali ya Kabul. Lengo la mazungumzo hayo kama ilivyodai Washington ni kuleta usalama ndani ya nchi hiyo iliyoathiriwa na vita nya ndani na pia kupunguza idadi ya askari wa Kimarekani nchini humo. Licha ya matamshi ya hivi karibuni ya Waziri wa Ulinzi wa Marekani ya kupunguzwa idadi ya askari wa nchi yake huko Afghanistan, hasa baada ya kufikiwa makubaliano tarajiwa na kundi la Taleban, lakini suala hilo halitokuwa na maana ya kuondoka kikamilifu askari hao wa kigeni katika nchi hiyo ya Asia. Hii ni kwa kuwa Rais Donald Trump amenukuliwa mara kadhaa akisema kuwa hata kama makubaliano kati ya nchi yake na kundi hilo yatafikiwa, uwepo wa kijeshi wa Marekani nchini Afghanistan hautofikia tamati. Tarehe 29 Agosti mwaka huu Trump akizungumza na kanali ya televisheni ya Fox News alielezea azma ya Marekani kuendelea kuwepo kiintelejensia nchini Afghanistan hata kama kutafikiwa makubaliano na kundi la Taleban.
Akijibu swali kuhusiana na iwapo askari wa Marekani walioko Afghanistan wataendelea kusalia nchini humo hata baada ya kufikiwa makubaliano tarajiwa na kundi la Taleban au la? Trump alisema: "Ndio, ni lazima tubakie huko kwa kiwango fulani na hilo ndilo tutakalofanya. Hata kama tutakuwa tumeipunguza idadi ya askari wetu, lakini tutaendelea kubakia huko daima." Misimamo ya kugongana ya rais huyo wa Marekani juu ya kuondoka askari wa nchi yake Afghanistan, katika hatua ya kwanza yanabainisha kutofahamika malengo na hatua za madola ya kigeni yakiongozwa na Marekani nchini Afghanistan na wakati huo huo yanaonyesha kuwepo tofauti ndani ya Marekani yenyewe kati ya Trump na muundo wa utawala wake kuhusiana na kadhia ya kuwepo askari wa nchi hiyo katika nchi hiyo ya Asia. Hadi sasa askari wa Marekani bado wapo Afghanistan na suala hilo linaonyesha kuwa na nguvu muundo wa kiutawala juu ya maamuzi ya White House kuhusiana na suala la kuendelea kubakia askari hao nchini Afghanitan kwa muda usiojulikana. Hata kama Trump anajitahidi aweze kushinda katika uchaguzi ujao wa rais wa Novemba 2020 kupitia mafanikio ya siasa za kigeni, suala la kuondoka askari wa Marekani huko Afghanistan ni moja ya nukta muhimu zinazopewa uzito na serikali yake. Pamoja na hayo, Trump hatafanikiwa kufikia matakwa yake hayo iwapo atashindwa kufikia makubaliano na kundi la Taleban.