Iran na Uturuki; washirika wawili wa kuaminiana katika wakati mgumu
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i56969-iran_na_uturuki_washirika_wawili_wa_kuaminiana_katika_wakati_mgumu
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Uturuki, kama nchi mbili jirani zina kiwango kizuri cha uhusiano katika nyuga mbali mbali hasa za kiuchumi na katika uga wa kieneo pia ni nchi mbili athirifu.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Oct 31, 2019 06:56 UTC
  • Iran na Uturuki; washirika wawili wa kuaminiana katika wakati mgumu

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Uturuki, kama nchi mbili jirani zina kiwango kizuri cha uhusiano katika nyuga mbali mbali hasa za kiuchumi na katika uga wa kieneo pia ni nchi mbili athirifu.

Katika miaka ya hivi karibuni, Iran na Uturuki zimechukua mkondo wa kuimarisha uhusiano wa kiuchumi kwa sababu ya nukta nyingi za pamoja za kiutamaduni, kihistoria na pia kutokana na mpaka wao wa pamoja. Nchi mbili zinalenga kuhakikisha kuwa mabadilishano yao ya kibiashara yanafika dola bilioni 30  kwa mwaka.

Kuundwa Baraza Kuu la Ushirikiano baina ya Iran na Uturuki, kuandaliwa kwa wakati vikao vya tume mbali mbili za kitaalamu baina ya nchi mbili hasa tume ya pamoja ya kiuchumi, tume ya pamoja ya uchukuzi na mawasiliano na kamati ya kistratijia ya kilimo na pia kuanza kutumika sarafu za kitaifa za nchi mbili katika mabadilishano ya kibiashara na kibenki ni mambo ambayo yamepelekea kuimarika kasi ya uhusiano wa Tehran na Ankara.

Kwa kuzingatia mchakato huu na irada ya viongozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Uturuki ya kuwa na uhusiano bora zaidi wa kiuchumi na kisiasa, kuna muelekeo bora katika mustakabali wa ushirikiano wa nchi hizi mbili.

Kuanza kutumiwa sarafu za kitaifa katika uhusiano wa mifumo ya kifedha ya Iran na Uturuki na hali kadhalika kuimarishswa uhusiano na nchi zingine ni mambo ambayo yatakuwa kwa maslahi ya nchi mbili na eneo kwa ujumla.

Iran na Uturuki zina uwezo mkubwa ambao haujatumika katika nyuga za nishati, kilimo, utalii, usafiri wa reli na mipaka ya pamoja. Uwezo huu ukitumika vizuri unaweza kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi wa pande mbili na hata kufikia malengo makubwa zaidi kuliko yale yaliyoainishwa katika kiwango cha mabadilishano ya kibiashara kwa mwaka.

Katika uga huu, Mahmoud Vaezi, Mkuu wa Ofisi ya Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran akizungumza Jumatano, 30 Oktoba katika sherehe za Siku ya Kitaifa ya Uturuki hapa Tehran alisema uhusiano wa nchi mbili ni wa kistratijia na kuongeza kuwa: "Iran na Uturuki zina nukta nyingi za pamoja za kiutamaduni na kihistoria na nukta hiyo ni rasilimali bora zaidi ya nchi mbili katika kuwa na uhusiano wa kiwango cha juu."

Uhusiano mzuri baina ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Uturuki hauhusu tu pande mbili bali pia Tehran na Ankara katika uga wa kieneo zina nafasi muhimu katika usimamizi wa mlingano wa kieneo.

Ushirikiano wa Iran na Uturuki katika mgogoro wa Syria katika fremu ya 'Mchakato wa Astana' sambamba na nafasi  ya Russia ni jambo ambalo limekuwa na matokeo athirifu katika kusaidia kufikiwa usalama na uthabiti unaokubalika Syria na katika eneo.

Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Russia na Uturuki

Utatuzi wa mgogoro uliojitokeza kaskazini mwa Syria na kufanyika kikao cha kwanza cha Kamati ya Katiba ya Syria mjini Geneva baada ya mazungumzo ya Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Russia na Uturuki ni kiashiria cha kuwa athirifu ushirikiano wa nchi hizi tatu.

Hassan Rouhani, Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, siku ya Jumatano alimtumia ujumbe wa pongezi Rais Reccep Tayyip Erdogan wa Uturuki kwa munasaba wa Siku ya Taifa ya nchi hiyo na kusisitiza kuwa: "Matukio ya muongo mmoja uliopita katika eneo na nafasi kubwa ya Iran na Uturuki katika kusaidia kutatua matatizo ya eneo ni ishara kuwa  kushirikiana nchi mbili kunaweza kudhamini usalama na amani pamoja na uthabiti katika eneo."