Bunge la Iraq laafiki kujiuzulu Waziri Mkuu Adil Abdul-Mahdi
(last modified Sun, 01 Dec 2019 13:38:58 GMT )
Dec 01, 2019 13:38 UTC
  • Bunge la Iraq laafiki kujiuzulu Waziri Mkuu Adil Abdul-Mahdi

Bunge la Iraq lililokutana kwa kikao cha dharura kilichofanyika leo limeukubali uamuzi uliochukuliwa na Waziri Mkuu wa nchi hiyo Adil Abdul-Mahdi wa kujiuzulu wadhifa wake huo.

Katika kikao hicho kilichohudhuriwa na akthari ya wabunge, kwa kutumia kifungu cha 75 cha katiba, bunge la Iraq sambamba na kukubaliana na uamuzi huo wa Abdul-Mahdi, limemtaka Rais Barham Salih awasilishe bungeni jina la kiongozi mpya wa serikali.

Siku ya Ijumaa, Adil Abdul-Mahdi alieleza katika taarifa maalumu aliyotoa kwamba, kutokana na hali iliyopo na ili kuepusha kuendelea machafuko yanayojiri nchini humo kutokana na maandamano ya upinzani ya wananchi, analitaka Bunge lichukue uamuzi kuhusiana na kuundwa serikali mpya. Abdul-Mahdi aliwasilisha barua yake rasmi ya kujiuzulu kwa Bunge jana usiku.

Bunge la Iraq likiendelea na kikao chake cha dharura

Katika kikao cha leo cha bunge, Spika Muhammad al-Halbousi alisema, kulingana na kifungu cha 76 cha katiba, Rais ana fursa ya muda wa mwezi mmoja kuwasilisha bungeni jina la waziri mkuu mpya.

Katika muda huo wa mwezi mmoja hadi litakapowasilishwa bungeni jina la waziri mkuu mpya, serikali ya Adil Abdul-Mahdi itafanya kazi kama serikali ya muda. Baada ya kupita muda wa mwezi mmoja, kulingana na kifungu cha 81 cha katiba ya Iraq, endapo rais atashindwa kumpata mtu anayefaa, ni yeye mwenyewe ndiye atakayefanya kazi za waziri mkuu hadi atakapopendekezwa mtu mpya wa kushika wadhifa huo.../