Mar 09, 2020 11:28 UTC
  • Bahrain yashinikizwa iwaachilie huru wafungwa wa kisiasa wanawake

Jumuiya ya ‘Amani Kwa Ajili ya Demokrasia na Haki za Binadamu’ imewataka viongozi wa Bahrain kutambua haki za wanawake na hivyo kuwaachilia huru wafungwa wote wa kisiasa wanawake ambao wanashikiliwa kwa kosa kueleza mitazamo yao ya kisiasa au kuwa ni wanaharakati wa haki za binadamu.

Jumuiya hiyo imesisitiza katika taarifa yake kwamba, utawala wa Bahrain wa Aal Khalifa umekuwa ukiwafuatilia na kuwatia mbaroni wanawake ambao ni wanaharakati wa masuala ya haki za binadamu na harakati za kisiasa.

Sehemu nyingine ya taarifa ya Jumuiya ya ‘Amani Kwa Ajili ya Demokrasia na Haki za Binadamu’ imefichua ukandamizaji na ubaguzi unaofanywa na utawala wa kifamilia wa Bahrain dhidi ya wanawake.

Bahrain ilianza kushuhudia harakati za wananchi dhidi ya utawala ulioko madarakani wa Aal Khalifa tangu Februari 14 mwaka 2011 huku ukandamizaji unaofanywa na utawala huo ukizitia hofu na wasiwasi fikra za waliowengi na taasisi za kutetea haki za binadamu ulimwenguni.

Kwa mujibu wa wanaharakati wa Bahrain, idadi kubwa ya shakhsia na viongozi wa makundi ya upinzani, madaktari, walimu, wanafunzi na wafanyakazi wa sekta ya umma wameshawahi kuteswa katika jela za nchi hiyo.

Utawala wa Aal-Khalifa unaoungwa mkono na nchi za Magharibi ikiwemo Uingereza na kwa msaada wa wanajeshi wa Saudi Arabia na askari usalama wa Imarati, ambao wametumwa nchini humo kwa kutumia mwavuli wa vikosi vya Ngao ya Kisiwa, unatumia njia na mbinu za ukatili mkubwa kukandamiza maandamano ya amani ya wananchi wa Bahrain.

Hadi sasa utawala wa Aal Khalifa umewatia nguvuni zaidi ya raia elfu kumi na moja wa Bahrain kwa tuhuma bandia, ambapo baadhi yao wamenyongwa na wengine wengi wamenyang'anywa uraia au kufukuzwa nchini humo.

Tags