Tahadhari ya makombora ya Sanaa dhidi ya Riyadh
Jeshi na makundi ya wananchi ya Yemen yamefanya mashambulizi ya makombora dhidi ya miji ya Riyadh na Jazan huko Saudi Arabia.
Tarehe 26 mwezi huu wa Machi vita vya Saudi Arabia na washirika wake dhidi ya Yemen viliingia mwaka wa sita huku kukiwepo habari kwamba, Serikali ya Uokovu wa Kitaifa, serikali iliyojiuzulu ya Yemen na muungano wa vita unaoongozwa na Saud Arabia wamekubaliana na pendekezo la kusitisha vita lililotolewa na Umoja wa Mataifa. Hata hivyo Saudi Arabia na washirika wake wameendeleza ukatili na mashambulizi dhidi ya taifa la Yemen.
Inaonekana kuwa, mashambulizi ya jeshi la Yemen na wapiganaji wa harakati ya wananchi ya Ansarullah dhidi ya miji ya Riyadh na Jazan huko Saudia yamefanyika kujibu uhasama na hujuma hizo za serikali ya Riyadh.
Msemaji wa jeshi la Yemen, Brigedia Jenerali Yahya Saree ametangaza kuwa, jeshi la nchi hiyo limezilazimisha ndege za kivita za Saudi Arabia zilizokuwa zimeingia katika anga ya mkoa wa Marib kurejea nyuma kwa kuzifyatulia makombora kadhaa. Saree amesema kuwa, makombora hayo yamezilazimisha ndege za adui zilizokuwa njiani kushamblia mji wa Sanaa kurejea nyuma na kuondoka katika anga ya Yemen. Jumapili ya jana pia Shirika la Mafuta la Yemen lilitangaza kuwa, Saudi Arabia na washirika wake wamezuia meli zilizokuwa zimebeba tani 112 za mafuta, tani 208 za dizeli, chakula, dawa na gesi kwa ajili ya matumizi ya nyumbani kutia nanga katika bandari ya al Hudaydah. Hii ni licha ya kuwa, Yemen inahitajia sana misaada ya kibinadamu kwa ajili ya kukabiliana na janga la maambukizi ya virusi vya corona.
Nukta kuhimu ya kuashiriwa hapa ni kwamba, japokuwa Saudi Arabia na washirika wake wamekubaliana na pendekezo la Umoja wa Mataifa la kusitisha mapigano nchini Yemen lakini kivitedo, nchi hizo haziheshimu suala hilo. Hali hii pia imekuwa ikikaririwa katika kipindi cha miaka mitano iliyopita ya vita vya Saudi na washirika wake dhidi ya taifa la Yemen. Kwa msingi huo harakati ya wananchi wa Yemen ya Ansarullah imefikia natija kwamba, suala la kusitisha vita ni mbinu inayotumia na wavamizi wanaoongozwa na Saudia kwa ajili ya kupoteza wakati, lengo likiwa ni kujipanga upya na kuimarisha vikosi vya mamluki na vibaraka wao katika maeneo mbalimbali kama al Jawf na Ma'rib wanakokabiliwa na mashinikizo makubwa na mbinyo wa jeshi la Yemen na makundi ya wananchi. Kwa kuzingatia ukweli huo jeshi la Yemen na washirika wake wameshambulia kwa makombora miji ya Riyadh na Jazan huko Saudia kama ujumbe unaosisitiza kwamba, mara hii taifa la Yemen halitatumbukia tena katika mtego na mchezo mchafu unaofanyika kwa jina la “kusitisha vita.”
Nukta nyingine tunayopasa kuashiria hapa ni kuwa, mashambulizi ya makombora dhidi ya miji ya Jazan na Riyadh ni aina fulani ya mashinikizo ya jeshi la Yemen na harakati ya Ansarullah dhidi ya Saudia. Kwa maneno mengine ni kuwa, jeshi la Yemen na harakati ya Ansarullah wanaiambia Saudia na washirika wake kwamba, iwapo hawataheshimu pendekezo la usitishaji vita la Umoja wa Mataifa na kuendeleza mashambulizi dhidi ya taifa la Yemen na kuingilia mambo ya ndani ya nchi hiyo, Wayemeni wanao uwezo wa kutoa dharba na pigo kali hata katika maeneo nyeti na muhimu kama mji wa Riyadh.
Kwa kutilia maanani hayo yote tunaweza kusema kuwa, mashambulizi ya makombora ya jeshi la Yemen na harakati ya Ansarullah huko Saudi Arabia ni tahadhari kwa utawala huo wa kifalme na washirika wake na ujumbe kwamba uhasama na uchokozi wao utakabiliwa na jibu kali.