Jul 23, 2020 13:00 UTC
  • Jumuiya 16 za kimataifa zaiandikia barua Bahrain na kuitaka isiwanyonge raia

Jumuiya 16 za kimataifa zimemuandikia barua mfalme wa Bahrain Hamad bin Isa bin Salman al-Khalifa zikimtaka azuie utekelezaji wa adhabu ya kifo dhidi ya vijana wawili kwa kosa la kuwashambulia polisi.

Katika barua hizo, taasisi hizo mbali na kutangaza upinzani wao dhidi ya adhabu ya kunyonga zimesisitiza kuwa, vijana hao walilazimika kukiri makosa baada ya kuteswa vibaya na vyombo vya usalama vya nchi hiyo.

"Vitendo vya mateso, ukandamizaji na adhabu ya kunyonga vinapaswa kukomeshwa nchini Bahrain", imesema sehemu moja ya barua hiyo ya taasisi za kimataifa.

Februari mwaka 2014 vikosi vya usalama vya Bahrain vilimtia mbaroni Hussein Ali Issa (33) na Muhammad Ramadahn (37) kwa tuhuma za kuwashambulia polisi na kushiriki katika mlipuko mmoja katika kijiji cha al-Deir kaskazini mwa mji mkuu Manama ambao ulipelekea kuuawa askari mmoja.

Mwezi Disemba mwaka huo huo Mahakama ya Jinai ya Bahrain ikawahukumu adhabu ya kunyongwa. Aidha mwaka 2015 Mahakama ya Rufaa iliidhinisha adhabu hiyo. Taasisi mbalimbali za haki za binadamu zinapinga kutekelezwa hukumu hiyo zikisema kuwa, kesi hiyo haikuendeshwa kiadilifu na hata kukiri makosa vijana hao kulitokana na mateso waliyopata.

Nchi ya Bahrain ni kisiwa kidogo kilichoko katika Ghuba ya Uajemi ambapo utawala wa kifamilia wa Aal Khalifa ndiyo unaotawala nchini humo. Dhulma, ukandamizaji, utumiaji mabavu na ubaguzi ni sifa kuu za watawala wa ukoo wa Aal Khalifa katika nchi hiyo ndogo ya Kiarabu.

Tags