Kikao cha kiistratijia cha Beirut, sauti moja ya Wapalestina
Makundi ya Palestina yameitisha kikao cha pamoja mjini Beirut, Lebanon na kulaani njama mbalimbali zinazofanywa dhidi ya Palestina na wamesisitiza kuwa kitu kimoja na kuendelea na muqawama katika kukabiliana na njama za Kiarabu/Kimagharibi na Kizayuni.
Katika radiamali yao ya kwanza kubwa dhidi ya makubaliano ya Umoja wa Falme za Kiarabu na utawala wa Kizayuni, makundi hayo ya Palestina yameweka pembeni hitilafu zao na juzi Alkhamisi yaliitisha kikao cha pamoja katika mji mkuu wa Lebanon, Beirut kikao ambacho kwa kweli kilikuwa muhumu sana kiistratijia.
Hicho kilikuwa ni kikao cha kwanza kabisa cha mshikamano mkubwa kama huo baina ya makundi ya Palestina katika kipindi cha miaka 20 iliyopita. Makatibu Wakuu na viongozi wa harakati 14 za Palestina wameshiriki kwenye kikao hicho huku Abu Mazen yaani Rais Mahmoud Abbas wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina akihutubia kikao hicho kutokea Ramallah kwa njia ya video. Kitendo cha viongozi wa makundi yote kushiriki katika kikao hicho na kuongozwa na Mahmoud Abbas kina maana ya kutangaza mshikamano na sauti moja ya Wapalestina wote mbele ya njama za Magharibi/Kizayuni/Kiarabu dhidi ya malengo matukufu ya Palestina. Katika hotuba yake kwenye kikao hicho, Rais Mahmoud Abbas amesema: Leo tumekusanyika pamoja kwa sababu sote ni taifa moja na malengo yetu ni mamoja. Palestina na Quds ndiyo iliyotushikamanisha na kutukusanya pamoja leo hapa.
Ushahidi mwingine wa umuhimu wa kiistratijia wa kikao hicho ni kuonesha kuwa makundi yote ya Palestina yamezielewa njama zinazofanywa dhidi ya taifa lao. Makatibu Wakuu na viongozi wa makundi yote ya Palestina wamesema kuwa kipindi inachopitia Palestina hivi sasa ni kipindi hatari mno ambacho hakijawahi kushuhudiwa mfano wake. Sasa hivi taifa la Palestina linakabiliwa na njama tatu kuu. Kwanza ni Muamala wa Karne, njama ambazo zimebuniwa na zinaendeshwa na Marekani na tayari baadhi ya vipengee vya njama hizo kubwa vimeshaanza kutekelezwa. Pili, ni kutekwa ardhi zaidi za Wapalestina, njama ambazo utawala wa Kizayuni unajigamba kwamba hakuna kinachoweza kuuzuia kuitekeleza. Hata hivyo kwa sasa hivi imeshindwa kuutekeleza kutokana na muqawama na mshikamano imara baina ya wananchi na makundi ya Palestina. Tatu ni kuweka uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni njama ambayo watekelezaji wake ni baadhi ya nchi za Kiarabu vibaraka wa Marekani. Ijapokuwa Imarati ndiyo iliyotangaza rasmi kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni wa Israel, lakini kitendo cha Saudi Arabia na Bahrain cha kuruhusu anga za nchi hizo zitumiwe na ndege za utawala wa Kizayuni zinazoelekea nchini Imarati ni ushahidi wa wazi kuwa nchi hizo nazo zimeanzisha rasmi uhusiano wa kawaida na wavamizi wa Quds.
Suala la tatu linalokifanya kikao cha makundi yote ya Palestina huko Lebanon kuwa na umuhimu mkubwa wa kiistratijia ni kupatikana mtazamo mmoja wa makundi yote ya Palestina kwa ajili ya kukabiliana na njama zinazolikabili taifa la Palestina. Makundi ya Palestina yametilia mkazo kufutwa makubaliano yote ya amani na mapatano yaliyofikiwa huko nyuma baina ya baadhi ya makundi ya Palestina na utawala wa Kizayuni wa Israel hasa mapatano ya amani ya Oslo. Makundi hayo yamehimiza pia kukatwa uhusiano wote na Marekani ambaye ndiye kiranja anayeongoza njama zote hizo tatu zinazoikabili Palestina hivi sasa. Kiujumla ni kwamba katika kikao hicho cha juzi Alkhamisi, makundi makuu ya Palestina yalisisitiza kwamba mshikamano na muqawama ndiyo njia pekee ya kuishinda Israel na njama hizo tatu za maadui wa Palestina. Katika kikao hicho cha Beirut, Ismail Hania, Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS alisema, jambo la kwanza kabisa linalopaswa kufanywa, ni kuiimarisha Palestina na kuirejeshea mshikamano wake wa kitaifa kwani msingi wa kuweza kupambana na kuzishinda njama zote ni umoja na mshikamano.
Amma ujumbe mkubwa uliotolewa na makundi yote ya Palestina kupitia kikao hicho cha Beirut ni kwamba nchi za Kiarabu ambazo zimeanzisha uhusiano wa kawaida na Israel, hata kama zinajifanya kuitetea Palestina, lakini hazifanyi mambo yao kwa hiari bali zinatii tu siasa na amri za Marekani.