Oct 08, 2020 02:38 UTC
  • Leo ni siku ya kumbukumbu ya Arubaini ya Imam Husain AS

Leo Alkhamisi inasadifiana na mwezi 20 Mfunguo Tano Safar 1442 Hijria, siku ya kumbukumbu ya 40 ya mjukuu wa Bwana Mtume Muhammad SAW, Imam Husain AS ambaye pia ni Imam wa Tatu wa Waislamu wa Kishia. Imam Husain AS na wafuasi wake 72 waliuliwa kidhulma na kikatili katika jangwa la Karbala la Iraq ya leo kwenye mwaka wa 61 Hijria.

Idadi kubwa ya Waislamu na wafuasi wa dini nyinginezo kwa miaka mingi huwa wanatembea kwa miguu kuanzia siku chache kabla ya 40 ya Imam Husain AS, kutoka mji wa Najaf kwa ajili ya kwenda kufanya ziara katika Haram na bwana huyo wa mashahidi huko Karbala.

Takwimu rasmi zinaonesha kuwa, mwaka uliopita, zaidi ya wafanya ziara milioni 18 walishiriki katika matembezi hayo ya Arubaini ya Imam Husain AS, matembezi ambayo yanahesabiwa kuwa ni mjumuiko mkubwa zaidi wa kidini wa kila mwaka duniani.

Matembezi ya Arubain ya Imam Husain AS maarufu kwa jina la Mashaya

 

Taarifa zinasema kuwa, wafanya ziara kutoka nchi 80 duniani hushiriki katika matembezi hayo ambayo ni maarufu kwa jina la Mashaya ambapo kwa upande wa watu wanaotoka nje ya Iraq, wafanya ziara kutoka nchini Iran ndio wanaounda asilimia kubwa zaidi ya wafanya ziara hao.

Mwaka huu lakini matembezi hayo yamefanywa na maashiki wa Imam Husain AS wa kona zote za Iraq tu bila ya kushirikisha wafanya ziara kutoka nje ya nchi hiyo kutokana na maambukizi ya kirusi cha corona.

Wapenzi wa Ahlul Bayt AS hapa nchini Iran ambao mara hii haikuyumkinika kwao kushiriki kwenye matembezi ya Arubaini ya Imam Husain AS huko Iraq, leo Alkhamisi watashiriki katika kumbukumbu hizi wakiwa majumbani mwao, kwa kusoma Ziara ya Arubaini ya mtukufu huyo na kujiunga na maashiki wenzao wa watu wa Nyumba Tukufu ya Bwana Mtume Muhammad SAW kote duniani na hasa huko Karbala Iraq.

Tags