Oct 08, 2020 11:53 UTC
  • Kwa nini wanaiogopa Siku ya Arubaini ya Imam Hussein AS?

Siku kama ya leo miaka 1381 iliyopita kwa mujibu wa kalenda ya Kiislamu, ilifanyika majlisi ya kwanza ya siku ya Arubaini tangu kuuawa shahidi mjukuu wa Mtume Muhammad SAW Imam Hussein bin Ali AS na watu wa Nyumba Tukufu ya Mtume ambao waliuawa shahidi tarehe 10 Muharram mwaka 61 Hijria.

Katika mkesha wa siku hii, Sayyid Hassan Nasrallah, Katibu Mkuu wa Harakati ya Hizbullah ya Lebanon ametoa hotuba muhimu na kusema: "Siku hii imekuwa ikiadhimishwa katika kipindi chote cha historia lakini katika zama hizi, utawala wa dikteta Saddam ulianza kuzuia maadhimisho ya Siku ya Arubaini na kuwapiga marufuku Waislamu wa madhehebu ya Shia kushiriki katika matembezi ya siku hii. Hata baadhi ya miaka, utawala  huo, ambao hatimaye ulipinduliwa, ulitumia ndege za kivita na helikopta kuwalenga wafanyaziara wa Imam Hussein AS. Swali ambalo linaibuka hapa ni hili kuwa, je ni kwa nini Arubaini ya Hussein AS inawaingiza hofu na wahka baadhi ya watawala na madola makubwa? 

Kuna sababu mbili muhimu ambazo tunaweza kuzitaja hapa.

Sababu ya kwanza ni muelekeo wa kimadhehebu wa Arubaini ya Imam Hussein AS.  Arubaini ni ibada ambayo kimsingi ni ya Waislamu wa madhehebu ya Shia ingawa inaadhimishwa pia na Masunni na pia wafuasi wa dini nyinginezo. Arubaini hufanyika kuwaenzi waliouawa shahidi Siku ya Ashura huko Karbala. Imam Hussein AS aliongoza mwamako  huko Karbala kwa lengo la kuulinda Uislamu na kuindoa dini hii katika makucha ya wanafiki ambao walikuwa wakitumia dini  kufikia malengo yao binafsi.  Ustadh Murtadha Mutahhari katika kitabu kuhusu Hamasa ya Husseini ameandika: "Athari kubwa zaidi ya tukio la Karbala ni kuwa pazia la unafiki liliondolewa na muelekeo wa kifalme ukaondolewa katika dini ya Mwenyezi Mungu."

Kwa hakika watawala wa ukoo wa Bani Umayya walikuwa wanatumia dini kufikia malengo yao ya kuwatawala Waislamu kiimla bila hata ya kuzingatia nguzo za awali kabisa za kidini.

Maadhimisho ya Siku ya Arubaini ya Imam Hussein AS huko Karbala Iraq

Katika dunia ya leo utawala wa ukoo wa Aal Saud unadai kuwa kiongozi wa ulimwengu wa Kiislamu na hivyo umejipachika jina la 'Wahudumu wa Maeneo Mawaili Matakatifu' yaani Makka na Madina, lakini kivitendo ukoo huo unaotawala Saudia umeingia vitani na nchi jirani ya Kiislamu yaani Yemen. Vita hivyo vimedumu kwa miaka sita na vingali vinaendelea ambapo mamia ya maelfu ya            Wayemen wameuawa na kujeruhiwa huku mamilioni wakiwa wakimbizi. Vita vya Saudia dhidi ya Yemen ni kwa maslahi ya maadui wa Uislamu.

Uislamu unaopigiwa debe na ukoo wa Aal Saud kwa uungaji mkono wa madola ya Magharibi yakiongozwa na Marekani ni 'Uislamu wa Kisekulari' ambao kimsingi unakiuka mafundisho matukufu ya Uislamu. Wanaounga mkono na kutetea 'Uislamu wa Kisekulari' wamechukua mkondo wa kuwa na uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni wa Israel ambao unatenda kila aina ya jinai dhidi ya taifa la Kiislamu la Palestina.

Mkabala wa 'Uislamu wa Kisekulari' ni Arubaini ya Imam Hussein ambayo ni kati ya vilelelezo vya Uislamu halisi ulioarifishwa na Mtume Muhammad SAW. Huu ni Uislamu wa mshikamano, udugu, amani, heshima kwa mwanadamu na ni Uislamu usiojua mipaka kama ilivyodhihirika katika Arubaini ya Imam Hussein AS. Kwa hivyo Arubaini ya Imam Hussein ni mfano wa namna Uislamu halisi unavyokabiliana na Uislamu wa kisekulari unaoungwa mkono na madola ya Magharibi. Ni kwa msingi huu ndio tunaona kunaenezwa propaganda mbali mbali za kupinga mjumuiko mkubwa wa mamilioni ya watu katika Arubaini ya Imam Hussein AS.

Nukta ya pili ni kuwa Arubaini imeweza kubakisha hai utambulisho wa kisiasa wa Ashura ya Imam Hussein AS. Ashura lilikuwa tulikio lenye mielekeo kadhaa ambapo muelekeo wake wa kisiasa ni nguzo muhimu ya harakati hii ya mjukuu wa Mtume Muhammad SAW.  Kufungamana na Wilaya au Mamlaka ya  Kiislamu na kupinga dhulma ni jumbe mbili za kisiasa za Ashura ya Imam Hussein AS. Wafuasi 72 wa Imam Hussein AS walisimama kidete mkabala wa jeshi la maelefu ya askari la Yazdi. Hatimaye waliuawa shahidi wakiwa wamesimama kidete kwa kutegemea mantiki ya Imam Hussein AS katika kukabiliana na Yazid na hicho kwa hakika ni kilele cha kufungamana na Wilaya. Hivyo mantiki ya kisiasa ya Ashura ilikuwa ni kupinga dhulma na kupambana na udhalimu.

Kiongozi wa Hizbullah Sayyid Hassan Nasrallah

Hujjatul Islam wal Muslimin Najaf Najafi Rouhani, mwakilishi wa Biitha (Ofisi) ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iraq anafafanua kuhusu nukta hiyo kwa kusema: "Utamaduni wa Ashura umeimarisha muqawama na mapambano. Ni huu utamaduni wa Ashura ndio uliongoza taifa la Iran katika miaka minane ya kujihami kutakatifu mkabala wa hujuma ya utawala wa Saddam. Ni huu utamaduni wa Ashura ndio ulioifanya harakati ya Hizbullah ya Lebanon ipate ushindi. Ni utamaduni huu huu ndio umepelekea harakati ya muqawama katika eneo kuweza kunawiri."

Leo wanaopinga muqawama na mapambano ya Kiislamu katika eneo la Asia Magharibi wanashuhudia kuimarika mhimili wa muqawama na kubadilika mlingano wa nguvu kwa maslahi ya mhimili huu. Kwa hivyo kujaribu kudunisha Arubaini ya Imam Hussein AS katika fremu ya vita vya vyombo vya habari na kuibua hitilafu baina ya nchi za eneo hasa baina ya Iraq na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni mkakati unaotekelezwa na maadui kwa malengo maalum.

Tags