Jeshi la Iraq lakomboa vijiji kadhaa mkoani Anbar
Wanajeshi wa Iraq na makundi ya wanamgambo waitifaki wamefanikiwa kukomboa vijiji kadhaa vya mkoa wa Anbar wa magharibi mwa nchi hiyo ambavyo vimekuwa vikishikiliwa na magaidi wa kundi la kitakfiri la Daesh au ISIS.
Taarifa zinasema katika oparesheni hiyo, jeshi la Iraq na wanamgambo wa kujitolea wamefanikiwa kukomboa vijiji vya lbu Khamis, Albu Khalid, Albu Asi na Albu Manahi ambavyo viko katika mji wa Fallujah.
Kwingineko kamanda wa oparesheni za kijeshi mkoani Anbar Ismail Mahlavi amesema magaidi 100 wa ISIS wameuawa katika kipindi cha siku chache zilizopita. Magaidi wa ISIS wangali wanadhibiti mji wa Fallujah ulio kilomita 50 maghairbi mwa mji mkuu Baghdad.
Kundi la kigaidi la Daesh liliteka maeneo mengi ya kaskazini na magharibi mwa Iraq mwezi Juni mwaka 2014 ambapo sanjari na kutenda jinai nyingi dhidi ya wananchi wa nchi hiyo, limefanya uharibifu mkubwa dhidi ya maeneo ya kihistoria, kidini na turathi za kiutamaduni zenye thamani kubwa za nchi hiyo. Hata hivyo hivi sasa jeshi na vikosi vya wananchi huko Iraq vimefanikiwa kukomboa maeneo muhimu kutoka kwa kundi hilo la kigaidi na kila leo habari zinaonesha kuzidi kulemewa kundi hilo la kitakfiri.